Hizi hapa faida, hasara kuandika majina ya watoto kwenye mali unazomiliki

Dar es Salaam. Umiliki wa mali ni jambo nyeti linalogusa vizazi na vizazi, huku wazazi wakizingatia kuacha urithi kwa watoto ili kuwahakikishia mustakabali wa maisha yao ya baadaye.

Miongoni mwa njia zinazotumika ni kuandika mali kama nyumba, viwanja au mashamba kwa majina ya watoto.

Hata hivyo, jambo hili lenye faida lakini linaweza kuwa chanzo cha changamoto katika familia.

Kufanya hivyo kunahakikisha urithi unakwenda moja kwa moja kwa watoto, kwa kuandika mali mapema kwa jina la mtoto, mzazi anapunguza uwezekano wa migogoro ya urithi baada ya kifo ikiwamo uporaji wa mali. Kwani katika baadhi ya jamii yapo matukio ya ndugu wa mzazi huchukua mali baada ya kifo chake, na kuwaacha watoto wakitaabika.

Kwa kuandika mapema, pia hupunguza mzunguko wa muda mrefu kufuatilia mirathi jambo linalopunguza gharama na muda.

Hata hivyo, hatua hii pia ina changamoto zake zikiwamo za matumizi mabaya ya mali, kwani mtoto anaweza kuuza au kutumia kwa namna atakavyo.

Pia, kunaweza kukakosekana udhibiti wa mali, kwa kuwa inapohamishwa mzazi hana nguvu ya kisheria kuizuia iwapo mtoto ataamua kuibadilisha umiliki, kuiweka rehani au kuiuza anapokuwa na umri wa miaka 18.

Mbali ya hayo, pale itakapotokea mzazi akahitaji kutumia mali hiyo kwa dharura (mfano kuuza nyumba kulipia matibabu), hataweza kufanya hivyo kwa kuwa atahitaji ridhaa ya kisheria ya mtoto.

Mzee Justin, mkazi wa jijini Dar es Salaam alifikwa na kadhia ya nyumba aliyomwandikisha mtoto kuuzwa akiwa ndani, kilichowajulisha kuwa imeuzwa ni notisi kuhusu uendelezaji wa eneo hilo.

Alipewa mwezi mmoja wa kuondoka kwa kuwa nyumba ilikwishauzwa. Jitihada za kuirejesha nyumba hiyo mikononi mwake ziligonga mwamba.

“Kila nilipokwenda nilishindwa kwa sababu nyumba niliandika jina la mwanangu, mwisho wa siku mimi na mke wangu tumerudi katika maisha ya kupanga nyumba, haikuwa matarajio yetu,” anasema Justin.

Akizungumza na Mwananchi, wakili Dominic Ndunguru anasema zamani watumishi wa umma walibanwa na maadili ya uongozi ambayo yaliwazuia kumiliki mali nyingi jambo lililowafanya kutafuta namna ya kuzificha, ikiwemo kuandikisha ndugu zao.

Anasema sheria hiyo iliumiza watu wengi na baadhi walipoteza mali zao baada ya wale waliowaandikisha kufariki dunia na ndugu kudai mali hizo hasa baada ya kutambua kuwa walimilikishwa.

Hali hiyo iliweka ugumu kisheria na mwisho mali ziliingia kuwa sehemu ya mirathi ya marehemu licha ya kuwa hawakuhusika katika kuzitafuta.

Anasema sasa mambo yamebadilika baadhi ya watu wanaandika watoto kukwepa kugawana mali na wenza wao pindi ikitokea migogoro ikiwemo ya ndoa inayoongezeka kila siku sambamba na ile ya kugombea mali za familia.

“Njia hii inazuia mali hiyo isifikiwe kiurahisi inapokuja suala la kugawana kwa sababu haipo chini ya umiliki wao wote,” anasema.

Anasema jambo hilo limeleta changamoto mpya, baadhi ya watoto wameanza kukengeuka na kudai umiliki wa mali hizo, mwisho wa siku wanauza na kuondoka jambo ambalo linawaumiza wazazi.

Wakili Onesmo Kyauke anasema kuandika majina ya watoto au mke katika mali, zikiwamo nyumba na viwanja inasaidia kuondoa matatizo mengi wakati wa mirathi mzazi anapofariki dunia.

Anasema hata mtu akiwa ameandika wosia kuna mlolongo mrefu, ikiwamo kwenda mahakamani ili kuuthibitisha na wakati mwingine kama haukuandikwa vizuri kunaweza kuwapo ucheleweshaji.

“Wengine wanaweza pia kuupinga wosia, lakini kama mali zimegawanywa kwa watoto kwa majina yao na mke, ikitokea umekufa hata zinapogaiwa hazihesabiwi kuwa ni maliza marehemu kwa sababu hazina umiliki wake,” anasema Kyauke.

Anafafanua ili kuepuka migogoro inayotokea baada ya mmiliki wa mali kufariki dunia njia hiyo inaweza kuwa nzuri.

“Hasara ipo ikiwa aliyeandikwa akiamua kuichukua, kama ni nyumba mzazi alikuwa anapata kodi labda kwa kupangisha mtoto akiamua kutaka kuanza kuchukua kodi hizo anaweza kisheria na mzazi anakuwa hana namna kwa sababu haipo kwenye umiliki wake na mtoto anakuwa na haki na mali hiyo. Hakuna sehemu yoyote anaweza kupinga hili,” anasema.

“Ili kuepuka hilo, mzazi anaweza kumilikisha mali watoto au mwenza wake akiwa hai na kuweka vigezo kuwa zitakuwa chini yao pindi atakapoondoka duniani, jambo litakalosimamiwa kisheria na kuwatoa katika hatari ya kupoteza mali zao.”

Wakili John Seka aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), anasema mali inayokuwa kwa jina la mtoto hata wanandoa wanapotalikiana hawawezi kugawana kwani haipo kwa majina yao.

Hiyo ni kwa mujibu wa sheria kama ambavyo mali husika haiwezi kuwekwa katika mirathi ya marehemu inapotakiwa kugawanywa kwa sababu haipo chini ya umiliki wake.

“Mali hii ni ya mtoto, sheria inamtambua kama mmiliki na mwenye uamuzi nayo atakapofikisha miaka 18 pekee,” anasema.

Wakati hili likiendelea kufanyika, wakili Nduguru anasema ujio wa vitambulisho vya Taifa (Nida) umekuja na ugumu wake hasa mzazi anapotaka kuandika jina la mtoto kwenye mali au biashara.

Hilo ni kwa sababu atatakiwa kuambatanisha kitambulisho cha muhusika ambacho kwa sasa kinatolewa kwa mtu aliyetimiza  miaka 18.

“Hata unaposajili kampuni, wengine walikuwa wanatoa hisa kwa watoto wao, siku hizi unatakiwa kuwa na Nida na Namba ya Mlipakodi (TIN) hali inayofanya mazingira kuwa magumu kwa watoto kuandikishwa katika baadhi ya vitu. Labda kama umenunua tu mtaani unaweza, ukienda kusajili rasmi lazima ufuate hili,” anasema.

Anasema huenda hilo likapatiwa ufumbuzi, kwani Serikali iko mbioni kuanza kutoa namba za utambulisho kwa watoto wadogo baada ya kukamilisha mradi wa majaribio katika wilaya 11 walizofanya nchini, ili kila mwananchi aweze kutambuliwa badala ya kusubiri afikishe miaka 18.

Wakili Ndunguru anasema ni vyema mtu ambaye atataka kufanya kitu kama hicho aombe msaada wa kisheria ili aelekezwe njia bora kusudi mali isije kupotea.

“Zipo njia za kulinda mtoto asije kuchukua mali ukiwa bado uko hai, ukisajili unaweka zuio kuwa nyumba hii ipo kwa jina la mtoto ndiyo, lakini itakuwa chini ya umiliki wake kamili pindi nitakapofariki dunia, unakuwa salama,” anasema.