Unguja. Ripoti ya utendaji kazi ya miezi sita ya Hospitali ya Wilaya ya Jitimai, imeonesha ongezeko kubwa la wagonjwa wanaohudumiwa, jambo linalozidi uwezo wa hospitali hiyo, huku sababu kuu ikitajwa kuwa ni kuimarika kwa huduma zinazotolewa.
Ripoti hiyo imesomwa leo Jumapili, Agosti 10, 2025 na Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk Lwayumba Lwegasha, katika kikao cha wadau wa afya kilichotumia mfumo mpya wa takwimu uliobuniwa na uongozi wa hospitali hiyo.
Dk Lwegasha amesema mfumo huo unalenga kuboresha uchambuzi wa changamoto na kutafuta ufumbuzi wa haraka.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Januari hadi Juni mwaka huu, hospitali ilipokea wajawazito 3,800 na watoto njiti 118, idadi inayozidi uwezo wa hospitali ambao ni kuhudumia wagonjwa 1,500 kwa mwezi. Aidha, wagonjwa wa nje waliopata huduma walifikia 56,211.
“Idadi hii ni kubwa mno ukilinganisha na uwezo wetu, lakini imechangiwa na maboresho makubwa tuliyoyafanya na ushirikiano na wadau wa sekta binafsi. Hata hivyo, bado tunahitaji msaada zaidi ili kuboresha huduma,” amesema Dk Lwegasha.
Ameeleza kuwa watumishi wa afya ngazi ya Jamii (CHW) wamechangia pakubwa katika kubaini matatizo ya utapiamlo kwa watoto katika shehia mbalimbali.
Pia amesema idadi ya wagonjwa waliopokelewa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) ilikuwa 163, hali inayoonesha hitaji la kuwa na ICU ya pili, mpango ambao tayari umeanza kufanyiwa kazi.
Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa damu, Dk Lwegasha amesema idadi kubwa ya wajawazito wanaofika hospitalini inaongeza mahitaji ya damu salama.
Hata hivyo, jitihada za kuongeza wachangiaji zimefanikisha ongezeko kubwa, kutoka chupa tano kwa wiki hadi chupa 100 kwa wiki.
Kwa upande wa manusura wa udhalilishaji, ripoti inaonesha kuwa 263 walipata huduma, kati yao wanawake 208 na wanaume 55, huku asilimia 10 pekee wakifika hospitalini ndani ya saa 72 za tukio.
Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Save the Children, Pius Ulaya amesema jamii inapaswa kuelimishwa zaidi kuhusu huduma zinazotolewa kwa manusura, ikiwemo msaada wa kisheria, kinga dhidi ya maambukizi na usaidizi wa kisaikolojia.
Naye Ofisa Uhamasishaji wa Damu Salama Zanzibar, Omar Said Omar amesema upatikanaji wa damu salama unahitaji jitihada za pamoja kutokana na kupungua kwa wachangiaji. “Mahitaji ya damu yanapanda huku wachangiaji wakipungua. Tunapaswa kuwathamini na kutumia lugha nzuri ili wasivunjike moyo,” amesema.