Kakolanya, Ambokile wavunja ukimya City

BAADA ya kipa Beno Kakolanya na mshambuliaji Eliud Ambokile kila mmoja kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Mbeya City katika msimu mpya wa mashindano ikiwa imerejea Ligi Kuu Bara, wachezaji hao wametoa neno wakisema wanaamini mbele yao wana kazi ngumu ya kuisaidia kufanya vizuri 2025-2026.

Msimu uliopita Kakolanya alisajiliwa na Singida Black Stars akitokea Simba, lakini baadaye alitolewa kwa mkopo kwenda Namungo ambako hakumaliza nayo msimu wakati Ambokile alikuwa sehemu ya kikosi kilichoisaidia City kurudi Ligi Kuu Bara baada ya kushuka nayo 2022-2023.

Kakolanya alisema: “Kurudi nyumbani kwangu ni faraja kubwa. Najipanga ili Ligi Kuu itakapoanza huduma yangu iwe msaada kwa timu kufanya vizuri. Pia natambua kutakuwa na ushindani wa dabi baina ya City na Prisons ambayo niliichezea mwanzo kabla ya kujiunga na Yanga.”

Kipa huyo wa zamani wa Yanga na Simba aliongeza: “Naitarajia ligi ijayo kuwa ya ushindani na ngumu. Kama mchezaji hilo linanipa nguvu ya kujipambanua katika mazoezi ya kuniweka fiti ili huduma yangu iifae timu.”

Mbali na hilo alisema upande wa makipa msimu ulioisha wazawa walifanya kazi nzuri akiwataja baadhi kuwa ni Patrick Munthari wa Mashujaa aliyemaliza na clean sheets 12, Yona Amosi wa Pamba (11), Yakoub Suleiman wa JKT Tanzania (8) na kwamba hilo linampa hamasa kwa upande wake ili kufanya vizuri zaidi. “Japo wageni ndio walikuwa vinara wa clean sheet kama Moussa Camara (19) na Djigui Diarra 17 na walionyesha ubunifu katika kazi zao, msimu ujao natarajia wazawa tufanye makubwa zaidi katika nafasi ya makipa,” alisema Kakolanya.

Kwa upande wake Ambokile alisema: “Msimu ulioisha nilikuwa na City Championship, hivyo nafahamu kwamba Ligi Kuu ni ngumu. Nitakuwa na kazi kubwa ya kutambulisha urejeo wangu kwa kufunga mabao ili kuisaidia timu kuwa katika nafasi nzuri.”

Mbeya City iliyowahi kutamba Ligi Kuu baada ya kupanda 2013 na kushuka 2023, imerejea safari hii sambamba na Mtibwa Sugar iliyoshuka misimu miwili iliyopita. Timu hiyo imerudi Ligi Kuu Bara baada ya kubeba ubingwa wa Championship.