Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri Mkuu na Kiongozi wa upinzani nchini Chad, Succès Masra amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kukutwa na hatia ya kueneza ujumbe wa ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni, njama ya uhalifu inayohusishwa na mzozo wa kijamii pamoja na kushiriki katika mauaji.
Masra ambaye ni rais wa chama cha Transformateurs ametakiwa pia kulipa faranga za CFA bilioni 1 kwa serikali ya Chad kama fidia.
Wakati wa hukumu hapo jana Agosti 9, 2025 baadhi ya mawakili wake walitokwa na machozi huku wakisema wamevunjika moyo, Francis Kadjilembaye, mratibu wa wanasheria wa Masra, amelalamikia dhuluma akisema:
“Mteja wetu amedhalilishwa tu. Amehukumiwa pamoja na raia wengine kwa msingi wa kesi tupu, kwa msingi wa kukosekana kwa ushahidi wowote, hii inasikitisha sana. Popote pale inapobidi, tutapaza sauti ilitasikika, tutaweka wazi kwamba mteja wetu ametendewa dhuluma ya wazi.”
Hata hivyo Wakili wa utetezi, Kadjilembaye, amewaambia waandishi wa habari baada ya uamuzi wa mahakama jana Jumamosi katika mji mkuu wa Chad, N’Djamena, kwamba Masra atakata rufaa dhidi ya hukumu yake.
Masra, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kati ya Januari na Mei mwaka jana, ni kiongozi wa chama cha Transformers na mkosoaji mkali wa Mahamat Deby, Rais wa sasa wa Chad.
Alishtakiwa pamoja na washtakiwa wengine 67, wengi wao wakiwa wa kabila moja la Ngambaye, kwa kusababisha mapigano kati ya wafugaji na wakulima Mei huko Logone Occidental, kusini-magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika ya kati. Mapigano hayo yalisababisha vifo vya watu 35 na wengine sita kujeruhiwa.
Masra amekanusha mashtaka dhidi yake, ambayo ni pamoja na hotuba ya chuki, chuki dhidi ya wageni na uchochezi wa mauaji ya halaiki.
Kabla ya kuondoka mahakamani, alitoa ujumbe kwa wafuasi wake: “Simameni imara.” Huku wanaharakati wa chama chake wakisema watatoa ujumbe maalumu kufuatia hukumu hiyo.
Kabila la Ngambaye lina umaarufu mkubwa miongoni mwa wakazi wa kusini, wengi wao wakiwa Wakristo na wapagani, ambao wanahisi kutengwa na mamlaka inayoongozwa na Waislamu huko N’Djamena. Kwa kumijibu wa Al Jazeera.
Masra aliwahi kuchuana na Rais Deby katika uchaguzi wa rais wa ulipita, ambapo Deby alishinda kwa zaidi ya asilimia 61.
Lakini Masra hakukubali matokeo, akidai kuwa kura ziliibwa. Baadaye alikubali kuhudumu kama Waziri Mkuu baada ya kusaini mkataba wa upatanishi na Deby.
Masra amepinga vikali watawala wa kijeshi walioingia madarakani nchini Chad Aprili 2021, baada ya kifo cha baba yake Deby, Idriss Deby Itno, ambaye alikuwa ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 30.
Deby alichukua madaraka mwaka 2021 na kuhalalisha urais wake kwa uchaguzi wa bunge mapema mwaka huu, ambao ulipingwa na Masra na chama chake.