Kumekucha mashindano ya Gofu ya Rotary Club

MASHINDANO ya 15 ya Gofu ya Rotary Club ya Bahari yanatarajiwa kufanyika Agosti 16 kwenye viwanja vya Klabu ya Gymkhana Dar es Salaam.

Mashindano hayo yatashirikisha zaidi ya wachezaji gofu 80 kutoka klabu mbalimbali kwa mujibu wa Rais wa Rotary Club ya Bahari, Dar es Salaam, Sameer Santosh.

Santosh alisema mashindano hayo yana lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya jamii.

Santosh alisema mbali ya wachezaji wa gofu, mashindano hayo yatashirikisha pia wadhamini mbalimbali.

“Maandalizi ya mashindano haya yanaendelea vizuri na tunawaomba wachezaji gofu kuendelea kujitokeza ili kufanikisha jambo hili. Mbali ya afya ambapo mpango wetu mkubwa ni kununua TVS za wagonjwa (TVS Ambulances) kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wa vijijini,” alisema Santosh.

Kwa upande Mkurugenzi wa Mahusiano wa Rotary Club ya Bahari Dar es Salaam, Bakari Machumu mpango wao pia ni kusaidia sekta ya elimu na mazingira.

Alisema wanatarajia kusaidia ufadhili wa masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi, na hisabati kama zana za kutatua changamoto za jamii.

“Tutasaidia kuboresha mazingira, ikiwa pamoja na kampeni ya upandaji miti, kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika shule na jamii na miundombinu ya afya,” alisema Machumu.

Alisema wanatarajia kukamilika kwa mradi wa kuchoma takataka Shule ya Msingi Tuangoma, utakaowanufaisha wanafunzi 3,000, wakiwamo 35 wenye ulemavu.

Alifafanua hadi sasa jumla ya wanafunzi zaidi ya 800 wamefaidika kupitia mashindano hayo kwa kupata mafunzo ya STEM Dar es Salaam na Zanzibar na vile vile wamefanikiwa kuongeza uelewa wa Saratani ya Shingo ya Kizazi.

Kwa upande wake, Rais mstaafu wa klabu hiyo, Fred Laizer alisema washindi watapata zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na safari ya Dubai kwa siku tatu na kucheza michezo miwili ya gofu, huku kukiwa na gari linaloshindaniwa kwa atakayepiga shimo moja kwa moja (hole-in-one).