Kuna uchaguzi wa Oktoba na ule wa nyumbani kwako

Dar es Salaam. Oktoba 2025 ndio hiyo inakaribia, muda wa uchaguzi mkuu. Na kama kawaida, hiki ndo kipindi ambacho kila mwanasiasa anataka kushinda tena kwa kishindo. Atachapisha mabango yenye sura yake na tabasamu kubwa, atahutubia mitaani kwa amsha amsha ya matumaini, atatoa ahadi za kuboresha maisha, za uongo na kweli, na atatumia kila dakika kujisafisha mbele ya macho ya wapiga kura wake ili wampe nafasi au wampe tena nafasi.

Lakini leo hatuzungumzii uchaguzi mkuu wa Tanzania. Tunazungumzia uchaguzi unaofanyika kimyakimya nyumbani kwako, bila Tume ya Taifa ya Uchaguzi, bila karatasi wala masanduku ya kupigia kura wala foleni — Uchaguzi wa Baba Bora.

Jiulize hivi; Kama leo hii familia yako, mkeo, watoto wako, wangekuwa na nafasi ya kuchagua upya mume au baba, wangekuchagua wewe tena? Na kama swali hilo ni kubwa, unaweza kulivunja vunja ili kupata majibu ya uhakika zaidi.

Jiulize, mkeo anaona nini kwako? Mkeo anajisikiaje kuwa na wewe kama mwenza wa maisha yake? Je, anakuona kama kiongozi wa familia au kama tatizo la familia?

Je, anakuogopa au anakuheshimu? Je, anapenda kuona unawahi kurudi nyumbani au anatamani kila siku uchelewe kutoka kazini ili ukifika ukute ameshalala?

Jiulize watoto wako wana mtazamo gani kuhusu wewe? Je, wanapotoka shule kurudi nyumbani wana shauku ya kutaka kufika, kukuona ili wakusimulie kila kilichotokea shule au ndio vile wanakuona kama mwalimu mwingine tu, tena mwalimu mnoko anayetembea na  fimbo nne nne mikononi.

Na hapa kwa watoto ndio kwa kupata majibu mazuri kabisa kwa sababu wenyewe hawana unafiki. Mtoto akikukubali anasema jambo, na akikukataa anasema jambo kubwa zaidi. 

Mtoto anapokukimbilia unapofika nyumbani, hiyo ni kura ya ndiyo. Lakini mtoto akikimbilia chumbani kila unaporudi hiyo ni kinyume chake.

Kama ambavyo kila uchaguzi unahitaji kampeni ndio na wewe pia unahitaji kufanya kampeni ili ukusanye kura za ndio nyingi hapo nyumbani.

Anza kampeni ya kumpa sikio mkeo, msikilize anapozungumza, sio unajifanya mjuaji kama google, kila akiongea unamkatisha, unatia sauti yako ili uonekane baba mwenye nyumba.

Anza kampeni ya kuomba msamaha unapokesea, wewe ni binadamu sio malaika, kila binadamu hukosea. Mwambie mtoto mke wako samahani unapokesea, mwambie mtoto wako nimekosea mwanangu unapokesa, na jitahidi usirudie tena. Maisha ya kuwa baba mbabe ya kizamani sana, yameshapitwa.

Kabla hujatoka nje kwenda kumpigia kura mgombea yeyote kwenye uchaguzi mkuu, hakikisha kwanza umeshinda uchaguzi wa ndani ya nyumba yako. Uchaguzi wa kuwa mume bora. Baba bora. Kiongozi wa kweli wa familia yako. Wapiga kura wa nyumbani kwako wakikukubali utayafurahia maisha kipindi chote cha uongozi wako.