Dar es Salaam. Umewahi kusikia baadhi ya watu ambao walikuwa na tabia hatarishi zilizowafanya wakakutana na watu mbalimbali, hata wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), lakini walipopimwa hawakubainika?
Wanasayansi wanatoa jawabu; watu hao wana ulemavu katika vinasaba vyao kwa kukosa vipokezi au vikombe sahani vijulikanavyo kama CXCR4 na CCR5.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu leo Jumapili, Agosti 10, 2025, Daktari aliyefanya tafiti kadhaa zihusuzo kirusi cha Ukimwi, Lilian Mwakyosi, amesema hitilafu hiyo huwasaidia kirusi hicho kushindwa kuingia katika DNA zao na mwishowe huondoka mwilini kama takamwili nyingine zinavyotoka.
Amesema VVU vinahitaji njia mbili za kuingia ili kupenya mwilini, na ikiwa njia moja imezibwa, virusi haviwezi kupenya.
“Katika maisha ya kibinadamu kuna watu ambao wana hitilafu ya kinasaba, ambayo katika seli zao hizi nyeupe, hawana hivi vipokezi vyenye uwezo wa kuruhusu kirusi cha Ukimwi kuingia katika seli hizi hai nyeupe. Hivyo mtu huyu hawezi kupata maambukizi ya VVU,” amesema.
Dk Mwakyosi, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Dare, amesema watu hao ni wachache sana na hakuna kwa sasa vipimo hapa nchini vinavyomsaidia mtu huyu kujua kama yeye ni miongoni mwa watu hao.
Pamoja na kundi hilo, amelitaja kundi la pili kuwa ni baadhi ya watu pale maambukizi yanapotokea, huwa wanakuwa katika hali tofauti za kinga, miili yao huwa na mapokeo tofauti kutokana na sababu mbalimbali za vinasaba.
Kuna baadhi ya watu wachache pia wameonekana na hali fulani, ambapo wanaweza kupata VVU lakini mwili wao una uwezo wa kudhibiti VVU visizaliane; vikabaki katika kiwango cha chini na haviongezeki.
“Ndiyo maana kuna watu unaweza kukutana naye akakwambia aligundua ana maambukizi mwaka 1997 na alikaa miaka mitatu, 10 na zaidi bila kutumia ARV.
“Hata hivyo, haimaanishi kwamba mtu huyu asitumie ARV. Ni muhimu kutumia ili asiendelee kuwaambukiza wengine, pia kinga inaweza kushuka na kumletea madhara,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyosi, watu hawa wamekuwa wakitumika zaidi katika kutafuta chanjo na tiba ya VVU.
“Wao, kirusi kikiingia mwilini na kuathiri seli, seli inatuma taarifa kuwa kuna shida, halafu mwili unatengeneza kinga tunaziita antibodies. Wale ambao wanapata maambukizi na kuna hitilafu nyingine huku zinazuia shambulio zaidi la seli zao, hao ndiyo watakuwa na antibodies na ndiyo ambao wamekuwa wakitumika zaidi kwenye upande wa kupata tiba na chanjo,” amesema.
Jinsi maambukizi yanavyotokea
Dk Mwakyosi ameeleza kwa kina namna kirusi cha Ukimwi kinavyoingia mwilini na kujizalisha, huku akifafanua kuwa huenda kujishikiza kwenye DNA na hiyo imesababisha ugumu katika kupata tiba yake.
Amesema kirusi kinapoingia mwilini mwa binadamu, huenda kujishikiza katika seli nyeupe za damu na ambazo huwa zinaathiriwa zaidi ni seli hai aina ya CD4, ukiacha nyingine nyingi tofauti.
“Kinachotokea, seli hizi huwa na vipokezi (vikombe sahani CXCR4 na CCR5) ambavyo vina uwezo wa kushikana na kirusi cha Ukimwi na kukiruhusu kujishikiza moja kwa moja kwenye seli na kuachia ‘content’ zake hapo.
“Hivyo, zikiingia kwenye seli, hupitia michakato tofauti inayoungwa mkono na enzymes za kubadilisha kiini kutoka RNA na kwenda DNA, ambapo hupata nafasi ya kuingia kwenye kiini cha seli ya binadamu. Kinapofanya hivyo, husababisha virusi vingi zaidi kuzaliana,” amesema na kuongeza;
“Kisha hutoka kwenye kiini cha seli vikiwa vimeshazaliwa vingi na kwenda kuambikiza seli nyingine. Hivi ndivyo maambukizi ya VVU hutokea pale kirusi kinapoingia katika mwili wa binadamu.”
Mtafiti wa virusi vya Ukimwi kutoka Kitengo cha Tiba ya Dawa, Chuo Kikuu cha Oslo, Profesa Dag Kvale, amesema virusi vinahitaji kipokezi cha ziada ili kupenya ndani ya seli lengwa ya CD4 na ikiwa kipokezi hiki hakifanyi kazi, maambukizi hayatokei.
“Watu wengine wana kasoro ya vinasaba katika kipokezi na wanaishi maisha ya kawaida kabisa, hawawezi kuonyesha kasoro yoyote. Kasoro hii ya jeni ipo kwa watu wengi duniani, lakini zaidi kwa waishio Ulaya Kaskazini,” ameeleza Kvale.
Kinyume na matarajio, kinasaba hiki chenye kasoro hakikusababishii ugonjwa, bali hukuzuia kuambukizwa VVU.
Kwa kuwa kinasaba cha CCR5 hakina uwezo wa kufanya kazi, virusi haviwezi kujifunga kwenye kipokezi hicho na huenda hapa ndipo siri ya kushinda virusi hivi ilipo.
“Tuna nakala mbili za kila jeni,” anasema Kvale na kuendelea, “Watu wenye kasoro kwenye vipokezi mshiriki katika nakala zote mbili za vinasaba hawaambukizwi VVU. Wale wenye jeni moja yenye afya na nyingine yenye kasoro huambukizwa kwa kasi ndogo na kupata maambukizi ya VVU yanayoendelea kwa taratibu zaidi.”
Maambukizi ya VVU hupatikana katika damu, manii, majimaji ya uke na maziwa ya mama, na ni nadra kuambukizwa kutokana na machozi, mkojo au mate ya mtu; aina hii ya majimaji hubeba virusi hivyo lakini kwa viwango vidogo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mmoja kati ya kila watu wanne ana VVU na mtu huyo hana habari. Hii inamaanisha watu milioni 9.4 wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa huo hatari.
Shirika la UNAids linasema asilimia 47 ya watu wote wanaoishi na VVU huwa wamedhibiti kiwango cha virusi hivyo mwilini kwa kutumia dawa na hivyo hawawezi kumuambukiza mtu mwingine.
Takwimu za Tume ya Kupambana na Ukimwi Tanzania (TACAIDS) zinaonyesha virusi vya ugonjwa huo vimewaathiri zaidi vijana wa kati ya miaka 14 hadi 25.