Lindi. Shirika la kimataifa la Sightsavers limetoa vifaa tiba vya kutolea huduma ya macho kwa Hospitali ya Rufaa ya Sokoine mkoani Lindi lengo likiwa ni kukabiliana na uhaba wa vifaatiba vya macho.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh56 milioni ni mashine ya B-scan ya macho, hadubini ya upasuaji, seti ya vifaa vya upasuaji, seti ya vifaa vya upasuaji mtoto wa jicho, lenzi ya 90D kwa uchunguzi wa retina, seti ya jezi ya majaribio, fremu ya majaribio kwa watu wazima na fremu ya majaribio kwa watoto.
Akizungumza leo jumamosi Agosti 9, 2025 wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Zuwena Omary amesema kuwa vifaa vilivyotolewa vitakwenda kumaliza changamoto ya malalamiko kwa wananchi wa Lindi ambao walikuwa wanakosa baadhi ya vipimo vya macho.
“Baadhi ya wananchi walikuwa wanakwenda kuhudumiwa katika hospitali za nje kutokana na kukosekana kwa baadhi ya vifaa vya kutolea huduma,niwaombe viongozi wenzangu kujitahidi kuvitunza na imani yangu kuwa wananchi hawatalalamika tena kwani vifaa vyote vya upimaji vimekamilika,” amesema Zuwena.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Sokoine mkoani Lindi Dk Shadrack Lusasi amesema vifaa tiba hivyo vitakwenda kuondoa changamoto kwa wagonjwa ambao walikuwa wanakosa baadhi ya vipimo kutokana na kukosekana kwa vifaa.
“Nawashukuru Shirika la Sightsavers kwa msaada wao wa vifaa tiba hivi,na matumaini yangu vifaa hivi vinakwenda kumaliza changamoto za wagonjwa wa Lindi kwani vifaa vyote vimetimia na sasa hakuna mgonjwa atakayekuwa anatoka Mkoa wa Lindi kwenda kwingine,” amesema Dk Lusasi.
Meneja wa mradi wa magonjwa yasiopewa kipaumbele Shirika la Sightesevers Peter Kivumbi amesema kuwa vifaa hivyo walivyovitoa vitasaidia kuondoa changamoto katika kutoa huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi.
Mkazi wa Lindi, Jasmine Kebwe amelishukuru shirika hilo kwa kuwaletea vifaa tiba vya kutosha na kusema kuwa hakuna mwananchi wa atakate toka nje ya mkoa huo kufuata huduma kwingine.
“Watu walikuwa wanatoka kwenda hospitali zingine nikwasababu baadhi ya vifaa vya kupimia vilikuwa hakuna, lakini baada ya kuletewa na hili shirika imani yangu kuwa changamoto itakuwa imekwisha na watu hawatakwenda sehemu nyingine,” amesema Kebwe.