Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imebatilisha uamuzi wa Kamati ya Taifa ya Mawakili, uliomtia hatiani rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi kwa kosa la ukiukwaji wa maadili ya kitaaluma.
Badala yake Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa Agosti 7, 2025 na jopo la majaji watatu, Elizabeth Mkwizu (kiongozi wa jopo), Awamu Mbagwa na Hussein Mtembwa, imeamuru kamati hiyo isikilize upya shauri lililokuwa likimkabili Mwabukusi lililomtia hatiani.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo kufuatia rufaa aliyoikata Mwabukusi akipingia uamuzi huo akidai kamati hiyo ilishindwa kutoa sababu za uamuzi wa pingamizi lililoibuliwa na Mwabukusi, badala yake ikaendelea kusikiliza shauri la msingi hatimaye ikamtia hatiani.
”Kwa kuzingatia hayo tunakubali rufaa hii,” imesema Mahakama hiyo katika hukumu iliyoandikwa na Jaji Mtembwa kwa niaba ya jopo, baada ya kujadili hoja za pande zote katika rufaa hiyo.
Baada ya kuikubali rufaa hiyo Mahakama hiyo imesema ingeweza kuamuru Kamati kutoa sababu za uamuzi na amri zake kuhusiana na pingamizi hilo, kisha kuendelea kusikiliza shauri kwa hoja zake kuu.
Hata hivyo, imesema inatambua mwenyekiti wa kamati hiyo aliyesikiliza na kutoa uamuzi wa shauri hilo ameshastaafu, haiwezekani kwa kamati ya sasa kuandika hukumu na kutoa sababu juu ya jambo ambalo haikulisikiliza.
”Kwa kuzingatia changamoto hii, tunalazimika kufuta mwenendo mzima wa kamati, amri juu ya pingamizi la awali yaliyotolewa na hukumu iliyolalamikiwa na amri nyingine yote yaliyotokana nayo,” imesema Mahakama hiyo na kuhitimisha.
Kwa hiyo, tunarudisha jalada la shauri kwa kamati ya awali ili lisikilizwe upya. Tunaamuru kila upande kubeba gharama zake mwenyewe.”
Mwabukusi alitiwa hatiani na kamati hiyo katika uamuzi wake ilioutoa Mei 17, 2024, katika shauri la maombi ya madai namba 10 ya 2023 ililofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) dhidi yake.
Katika shauri hilo, AG alimlalamikia Mwabukusi kutumia lugha isiyofaa kinyume na Kanuni za Mawakili (Utovu wa Maadili) za mwaka 2018.
AG alimshtaki Mwabukusi katika kamati hiyo kutokana na maneno aliyoyatamka Julai 3, 2023, wakati wa mwenendo wa kesi ya Mkataba wa Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Falme za Kiarabu za Dubai (Inter-Governmental Agreement – “IGA”),
Kesi hiyo ilifunguliwa na Alphonce Lusako na wenzake dhidi ya AG na wenzake, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mbeya, wakipinga mkataba huo kwa madai haukuwa na masilahi kwa Taifa, kesi ambayo Mwabukusi alikuwa mmoja wa mawakili wa wadai.
Katika Kamati hiyo AG alidai katika viwanja vya Mahakama hiyo, Mwabukusi baada ya kesi hiyo kuahirishwa, aliwakusanya watu na kuwahutubia akitumia maneno ya utovu wa maadili ya taaluma ya uwakili, yafuatayo.
”Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hawajui walichopitisha bungeni, kwamba hata Chifu Mangungo anasingiziwa maana yeye alijua ni mkataba.
Serikali imekuwa ikiwadanganya wananchi imesaini makubaliano na siyo mkataba.
Mgogoro ukizuka, kimbieni kufungua kesi nje ya nchi kwa sababu ukifungua nje ya nchi, position ya Uingereza haitambui sheria za Tanzania.
Kwa hiyo hata kama mtu amekiuka Sheria ya Maliasili (Natural Resources), akienda kule akisimama Uingereza, Natural Resources kule ni takataka, haiwi enforceable, kwa hiyo wanachofanya ni kujaribu kupotosha wananchi.
”Fuatilieni hansards (kumbukumbu za mijadala) za Bunge, ndipo mtagundua kwamba hakuna spika, mtagundua kwamba hamna waziri.
“Mtagundua kwamba kwa sababu kama spika mwenyewe alikuwa hajui anapitisha kitu gani, waziri alikuwa hajui anasaini kitu gani, ujue kwamba Chifu Mangungo was a genius.
“Mbarawa na Katibu Mkuu wake waondoke katika ile nafasi, wanahatarisha mali za Tanganyika, narudia kupigia mstari, wanahatarisha mali za Tanganyika siyo mali za Zanzibar, yaani kwenye Muungano kuna mali za Zanzibar na mali za Tanganyika.
“Mali za Zanzibar wamebaki nazo kule, za Tanganyika zikawekwa chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kwa hiyo walichokifanya ni kuchukua mali za Tanganyika na kuikabidhi bila kikomo kwa mtu, ndiyo maana hukuti mtu yeyote anayetujibu anaonesha anakujibu kwa kifungu gani,”alidai Mwabukusi.
Alidai Bunge kwa makusudi liliamua kusimamisha akili zake, utashi wake na uadilifu wake kwa mahaba ya mtu na wakasema mkataba huu ni wa mtu na kupitia mkataba huu, yeyote atakayeupinga, ni adui wa mtu huyo.
Hata hivyo, Mwabukusi alikanusha vikali tuhuma hizo kupitia hati ya kiapo cha majibu, akidai kwa kutamka maneno hayo, hakufanya utovu wa maadili ya kitaaluma.
Kamati hiyo katika uamuzi wake iliridhika maneno aliyotamka hadharani yalikuwa ni utovu wa maadili ya kitaaluma.
Hivyo, ilimtia hatiani kwa kosa hilo, lakini ikamwonya kuepuka kutumia maneno yasiyofaa, zaidi bali azingatie na kufuata maadili yake ya kitaaluma.
Mwabukusi hukuridhika na uamuzi huo, hivyo akakata rufaa hiyo Mahakama Kuu. Katika rufaa hiyo namba 14345 ya 2024 alitoa sababu 10.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika hukumu yake imezingatia sababu moja tu, Kamati kutokutoa sababu za uamuzi wa pingamizi la Mwabukusi.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo iliyosikilizwa kwa njia ya maandishi, Machi 24, 2025, Mwabukusi aliwakilishwa na Wakili Edson Kilatu.
Wakili Kilatu alidai mwenendo mzima mbele ya Kamati ya Mawakili ulipotoka kwa kukiuka kanuni hii ya msingi kuanzia kwenye kusikilizwa pingamizi la awali.
Alidai kamati ilitumia dakika kumi tu kujadili na kutoa uamuzi uliotokana na hoja zilizowasilishwa kwa siku nzima bila kutoa sababu za uamuzi wa pingamizi hilo hadi rufaa hiyo inasikilizwa.
Aliongeza kushindwa kutoa sababu za uamuzi kunakiuka haki ya kusikilizwa kwa usawa, na hivyo kuibua maswali kuhusu nia iliyosababisha kuharakisha kutoa haki.
Akijibu hoja hiyo Wakili wa Serikali, Ayoub Sanga alikiri kutoa sababu za uamuzi ni kinga dhidi ya uamuzi wa kiholela.
Hata hivyo, alieleza pia ni utaratibu wa kawaida wa mahakama kutoa uamuzi na kutoa sababu baadaye.
Kamati ilieleza baada ya kuwasikiliza wahusika, iliamua pamoja na mambo mengine kuwa sababu ya pili na ya nne za pingamizi la awali zimekataliwa
Ilieleza kuwa sababu za uamuzi huo kwenye pingamizi hilo zingetolewa wakati wa hukumu ya shauri la msingi na ikaamuru kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo siku iliyofuata na ikatoa uamuzi huo uliopingwa.
Hata hivyo, imesema kuwa kutokutoa sababu za uamuzi ni ukiukaji wa kanuni ya msingi ya haki ya kusikilizwa kwa usawa.
Badala yake imesema kuwa kutoa sababu ni sharti la msingi la haki na ni muhimu kwa kuridhisha pande husika.
Imesisitiza kutoa sababu kunadhihirisha uwajibikaji na uwazi na kunamuweka mtoa uamuzi wazi kukosolewa, hivyo kuhakikisha kwamba madaraka hayatumiki vibaya au kiholela.
“Kwa muktadha huu, Kamati ilikuwa na makosa na kwa kufanya hivyo, ilikiuka kanuni ya msingi ya haki ya kusikilizwa, ambayo ni ya msingi katika mchakato wa haki,” imesisitiza Mahakama na kuhitimisha:
“Hivyo, kwa kuwa dosari katika shauri hili imeathiri haki ya kusikilizwa, tunaona kuwa kasoro hiyo ilikuwa ya kimsingi na imeharibu mwenendo mzima wa shauri. Kwa hiyo, malalamiko ya mrufani kwa Kamati kutokutoa sababu za uamuzi yana mashiko.”