Dar es Salaam. Tofauti ya maisha ya bungeni ya aliyekuwa Spika, hayati Job Ndugai na spika mstaafu, Anna Makinda ni ya kipekee, lakini wamehudumu katika vyeo vinavyofanana.
Kwa mujibu wa Makinda, maisha yake na Ndugai yalikuwa mithili ya mtu na mdogo wake, kila wadhifa alioupata akiwa bungeni, mwanasiasa huyo alikuwa msaidizi wake na baadaye kurithi kabisa cheo husika.
Ndugai amefariki dunia saa 9 alasiri ya Agosti 6, 2025 katika Hospitali jijini Dodoma baada ya shinikizo la damu kushuka kupita kiasi, hali iliyosababishwa na maambukizi makali kwenye mfumo wa hewa.
Makinda ameyasema hayo jijini Dodoma leo Jumapili, Agosti 10, 2025 alipokuwa akitoa salamu zake katika hafla ya kitaifa ya kuaga mwili wa Ndugai, iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge.
Makinda amesema walikutana bungeni akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira, Ndugai alikuwa makamu wake.
Hatua hiyo, amesema ilikuja baada ya kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge, kisha Ndugai akachaguliwa kuwa mrithi wake kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Maliasili na Mazingira.
Baadaye, amesema alichaguliwa kuwa Naibu Spika, huku Ndugai aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge, akichaguliwa kumrithi.
Haikuishia hapo, amesema alipochaguliwa kuwa Spika, Ndugai akawa Naibu Spika na hata alipoacha wadhifa huo, Ndugai alimrithi katika nafasi ya uspika.

“Nilipokuwa Spika kuna kipindi fulani mlezi wake aliyemlea alifariki, tulikwenda kumzika Kongwa. Baada ya hapo nikakutana na dada yake, akaniuliza kwa hiyo na uspika utatuachia, nikamwambia nitawaachia, ndiyo hivyo, baadaye akawa Spika,” amesema
Amesema Ndugai alikuwa mwenye akili na mbunifu na walishirikiana kufanya mambo mengi ambayo kwa siku hizi Serikali imeamua kuyatungia sheria.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha yake, hakika sifa zote walizosema viongozi wa dini zinamstahili,” amesema.
Kwa upande wa Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju amesema amemtambua Ndugai alipokuwa Katibu binafsi wa Waziri wa Katiba na Sheria wa wakati huo, Harith Mwapachu akishinikiza kujengwa kwa Mahakama Kongwa.
Amesema alikuwa anakwenda mara kwa mara kwa waziri huyo ili Mahakama hiyo ijengwe na alifanikiwa kwani ilijengwa.
Amesema ataendelea kumuenzi kwa sababu ya mchango wake wa kupenda haki.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema atamkumbuka Ndugai kwa nidhamu yake ya kushiriki vikao vya ushauri wa mkoa (RCC), kwani ndani ya miaka mitatu hakuwahi kumwona kiongozi huyo akiacha kushiriki kikao chochote.
Amesema atamkumbuka kwa mchango wake katika mapinduzi ya elimu hasa mkoani humo, ndiyo maana umekuwa mkoa ulioshika nafasi ya pili na hatimaye ya kwanza nchini.
Amesema atamkumbuka kwa mapenzi yake kwa kilimo, akihimiza zao la korosho kiasi kwamba aliwahamasisha wengi walilime.
Ndugai aliyefariki dunia akiwa na miaka 62. Alizaliwa Januari 21, 1963, katika Kijiji cha Laikala, Kata ya Sagara, Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma. Amekuwa Mbunge wa Kongwa kuanzia mwaka 2000 hadi Agosti 3, 2025 lilipovunjwa.
Katika kura za maoni ndani ya CCM, Ndugai aliongoza na alikuwa anasubiri vikao vya uteuzi. Ndugai ameacha mke, watoto na wajukuu. Mwili wake utazikwa kesho Jumatatu Agosti 11, 2025, Kongwa.
Endelea kufuatilia Mwananchi