Maji yanapogeuka adui mtoa uhai

Dar es Salaam. Ingawa maji ni msingi wa maisha na maendeleo ya binadamu, yanapokosa usimamizi salama huweza kubadilika na kuwa tishio kwa uhai.

Kutoka kwenye visima vya nyumbani hadi kwenye mito, maziwa na bahari, mamia hupoteza maisha kila mwaka; wengi wao wakiwa watoto na vijana wenye umri wa mwaka mmoja hadi 24 duniani kote hali inayoonyesha kile kinachotegemewa kuokoa, pia kinaweza kuangamiza endapo tahadhari hazitachukuliwa.

Si huko pekee, majumbani imeshuhudiwa watoto wakipoteza maisha kwa kufa maji kwenye majaba, makaro na hata madimbwi.

Katika tukio la wiki iliyopita, Said Sihaba Khamis (18) alikufa maji, huku watu wengine watatu wakinusurika baada ya mashua kuzama katika Bahari ya Hindi walipokuwa wakielekea Unguja kwa shughuli za kibiashara.

Mashua hiyo ilikuwa na watu wanane kati ya hao watatu walijiokoa na wengine wanne hawakuonekana mara moja.

Aliyenusurika, Said Hassan Makame (16), mkazi wa Muambe anasema mashua hiyo ilipigwa na wimbi ndipo ikazama.

Mbali ya tukio hilo, mengine yaliyowahi kuripotiwa na Gazeti la Mwananchi na mitandao yake ya kijamii mwaka 2024 na 2025 ni pamoja na la Agosti 3, 2024 la kijana wa miaka 21 kuzama Mto Ngerengere, mkoani Morogoro alipokuwa akiogelea. Juhudi za uokoaji zilichukua takriban saa nane hadi mwili wake ulipoopolewa Agosti 4, 2024.

Mei 2024, mashua ilizama katika Mto Ukingwamizi, wilayani Mlele, mkoani Katavi na kusababisha vifo vya wanaume wanne.

Septemba 26, 2024 katika Ziwa Victoria, mtumbwi ulizama na watu 29 waliokolewa.

Vilevile, Agosti 2024 katika ziwa hilo mtumbwi ulizama na mtu mmoja alipoteza maisha. Januari 17, 2025 mwanaume mwenye miaka 41 alizama kisimani akijaribu kumuokoa mbuzi, mwili wake uliopolewa Januari 17, 2025.

Aidha, kuna matukio ya Septemba 20, 2018 ambapo Kivuko cha MV Nyerere kilichokuwa kinafanya safari kati ya Bugolora na kisiwa cha Ukara, Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza kilizama na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 230.

Mei 21, 1996, MV Bukoba iliyokuwa ikitoka Bukoba, mkoani Kagera kwenda jijini Mwanza ilizama katika Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 800.

Novemba 6 mwaka 2022, ndege ya Precison Air iliyokuwa ikitoka jijini Dar es Salaam kwenda Bukoba ikiwa na abiria 43 kati yao 39 walikuwa abiria, marubani  wawili na wahudumu wawili ilianguka ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 19 na 24 kuokolewa.

Mbali ya matukio hayo yaliyoripotiwa, yapo mengine ambayo hutokea pasipo umma kujulishwa.

“Sitasahau siku niliyochukua familia yangu na kwenda ufukweni kupunga upepo wa bahari kutokana na ombi la mtoto wangu ambaye sikujua kwamba nakwenda kumpoteza,” anasema Zainabu Bakari, mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam.

Anasema mtoto wake, Abubakar Makame (12) alimuomba waende baharini kwa kuwa wanaishi jirani, hivyo pamoja na wanafamilia wengine walikwenda.

Wakiwa huko, wimbi la maji lilipiga na kumsomba mwanaye ukawa ndio mwisho wake duniani.

“Kwa sababu haikuwa siku ya sikukuu tulikuwa wachache tuliokwenda na hatukuwa na ujuzi wa kuogelea, hivyo mwanangu alikuwa anapiga kelele kuomba msaada hata alipojitokeza wa kwenda kumsaidia alikuwa tayari keshapoteza maisha,” anasema.

Takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2021 zinaonyesha takriban watu 3,000 hufariki dunia kila mwaka nchini Tanzania kutokana na ajali za kuzama majini, huku watoto wenye umri chini ya miaka 14 wakiwa katika hatari zaidi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) kupitia WHO kuhusu kuzuia vifo vinavyotokana na kuzama majini ya mwaka 2024, zaidi ya watu 236,000 hufariki dunia kila mwaka duniani kutokana na kuzama maji, huku asilimia 90 ya vifo hivyo vikitokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, Tanzania ikiwamo.

Ripoti inaeleza kuzama majini ni sababu ya tatu inayoongoza kwa vifo vya ajali zisizokusudiwa na inachangia asilimia saba ya vifo vyote vinavyotokana na majeraha.

Inaelezwa kwenye ripoti hiyo, Afrika inaongoza kwa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha vifo vya kuzama maji duniani vikiwa 5.6 kwa kila watu 100,000.

Ripoti inatahadharisha kama hali itaendelea ilivyo, watu zaidi ya milioni 7.2, wengi wao wakiwa watoto wanaweza kufa kwa kuzama majini kufikia mwaka 2050.

Ni kutokana na madhila hayo, Siku ya Kuzuia Kuzama Maji Duniani ilitangazwa rasmi Aprili, 2021 kupitia Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na huadhimishwa Julai 25 ya kila mwaka.

Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Makao Makuu, John Nyanda anasema hakuna takwimu sahihi za kitaifa zinazoonyesha ukubwa wa tatizo la watu kuzama majini, hivyo ni vigumu kukadiria kiwango halisi cha vifo.

Hata hivyo, anasema matukio hayo yanaweza kuepukwa endapo jamii itachukua tahadhari mapema na kuboresha mazingira hatarishi.

“Hili ni jambo ambalo tumekuwa tukikumbana nalo, mengine ni kutokana na uzembe wa wazazi na walezi na mengine ni kutokana na kutokuwa na mazingira salama ya kufanyia kazi,” anasema.

Anasema jeshi hilo linaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu usalama majini na maeneo mengine kupitia shule, mikusanyiko ya watu na kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa.

Amesema jeshi hilo lina askari waliopatiwa mafunzo maalumu ya uokoaji majini wakiwa na vifaa vya kisasa vya uokoaji.

Anatoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha chemba na visima vinafunikwa kwa mifuniko imara, huku wale wenye mabwawa ya kuogelea wahakikishe watoto hawaendi maeneo hayo pasipo uangalizi.

“Kazi hii si yetu pekee, tunahitaji ushirikiano wa serikali za mitaa, walimu, vyombo vya habari na hata wamiliki wa boti kuhakikisha maeneo waliyopo yanakuwa salama na uwepo uangalizi kwa watoto ili kuokoa maisha ya Watanzania,” anasema.

Anasema jeshi hilo hupokea taarifa za dharura kupitia namba ya simu 114 inayopatikana bure kwa saa 24.

Mbali ya jeshi hilo, serikali za mitaa pia zimekuwa zikitoa elimu na tahadhari kwa wananchi ili kuzuia vifo vinavyotokana na kuzama kwenye visima, makaro ya maji machafu, mito na bahari.

Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Feri, Juma Mwingamno anasema wamejikita kutoa elimu na pia hufuatilia ujenzi wa chemba na visima kwenye makazi ya wananchi.

“Tumejikita zaidi kutoa elimu ya usalama kwenye maeneo yetu. Tunakataza watu kuacha mashimo wazi, kwani yanaweza kusababisha ajali, hasa kwa watoto,” anasema.

Kwa maeneo ya fukwe za bahari anasema wameanzisha vikundi vya usimamizi wa rasilimali za uvuvi (BMU) vinavyotoa elimu na baadhi ya maeneo hatarishi yamefungwa.

“Tunawaelekeza wazazi wasiruhusu watoto kuingia baharini bila uangalizi wa watu wazima… tumefunga maeneo hatari kama yenye kina kirefu cha maji,” anasema.

Kamanda wa Kikosi cha Polisi Wanamaji, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Moshi Sokoro anasema; “Tumekuwa tukitoa elimu kwa wavuvi kuzingatia hali ya hewa na waache kutumia mazoea, kwani taarifa huwa zinatolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa. Waache visingizo kuwa hawajajua kwani taarifa zinapatika kwa njia mbalimbali.

Kwa wazazi na walezi, anasema wanapaswa kuwa makini wanapokuwa nao kwenye fukwe.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Usimamizi wa Maafa, Suleiman Kova anasema watu wanatakiwa kuwajibika zaidi katika matumizi ya vyombo vya usafiri wa majini, akieleza ajali za majini ni hatari sawa na zile za barabarani, lakini wengi huzichukulia kwa wepesi.

“Watu wengi wanadhani ajali ni zile za barabarani tu, lakini ajali za kwenye maji nazo zina madhara makubwa mno,” anasema Kova aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi wa mikoa mbalimbali nchini ukiwemo wa Dar es Salaam.

Anasema vifo vinavyotokea kwenye maziwa, bahari, mito na hata visima, vinaacha athari kubwa kwa familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

“Kama kuna abiria 60 kwenye boti, halafu ikizama, wote wakifa huo ni msiba wa kitaifa, lakini watu hawafanyi maandalizi ya kiusalama kama inavyofanyika kwa magari,” anasema.

Kova anasema kabla ya kuanza safari, boti au chombo chochote cha majini kinapaswa kukaguliwa, kifanyiwe matengenezo na kiwe na vifaa vyote vya uokoaji kama jaketi za kujiokoa, taa, radio za mawasiliano na vingine.

Pia anasema ni lazima kuwe na watu waliopata mafunzo maalumu ya uokoaji kwenye vyombo vya majini, watu kujifunze kuogelea kuanzia watoto kwa sababu ajali haina taarifa.

Anashauri; “Ajali ikitokea, mtu asibaki kushangaa tu, anatakiwa aingie majini kusaidia. Siyo kila mtu anaweza, lakini lazima kuwe na walio tayari kwa hilo kwa kuwafundisha watoto kuogelea hata kwenye mabwawa, siyo tu kwa ajili ya mashindano.

Anasema kuna watoto wanazama visimani, hivyo familia lazima zichukue hatua kwa kuvifunika, kuweka uzio, wasisubiri hadi mtoto afe ndipo hatua zichukuliwe.

Daktari wa magonjwa ya dharura katika Hospitali ya Aga Khan, Hussein Manji anasema wamekuwa wakitoa elimu kwa sekta mbalimbali kuhakikisha wanasaidia watu wanaokumbana na ajali za kwenye maji kwa kuwapa huduma ya kwanza.

“Hivi karibuni tulipokea mtoto alizama baharini, tulihakikisha tunaokoa maisha yake kwa kumpa huduma ya kwanza na kila jambo la hatari halitokei, huku tukiendelea kutoa elimu ya kuwasaidia watu kwenye ajali za maji,” anasema.

Anasema pia walimpokea kijana mvuvi kutoka Kisiwa cha Mbudya, ambaye kwa bahati mbaya alichelewa kupata huduma sehemu aliyotolewa, hivyo alifikishwa hospitalini akiwa ameshafariki dunia.

Huduma ya kwanza kwa mtu aliyezama majini inalenga kuokoa maisha haraka, kurejesha upumuaji na kuzuia madhara zaidi kabla ya msaada wa kitabibu kufika.

Nyanda kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji anasema kamba na mti hutumika katika uokoaji kutegemea mazingira akitoa mfano vijijini ambako hakuna maboya.

“Tunasema njia hizi zinakuwa salama kwa mfano kwenye mito, tunashauri kama mtu atarushiwa kamba au kuvutwa na mti anaposogea mwokoaji awe na jaketi la uokozi kwa ajili ya usalama wake kabla ya kutoa msaada wowote kwa mwingine,” anasisitiza.

“Haishauriwi mtu asiyejua kuogelea au asiye na usalama wa kutosha kujitosa majini kufanya kazi ya uokoaji.

“Anapaswa kumvuta aliyezama hadi eneo salama kwa kutumia kifaa au kuogelea akiwa amemshika vema.”

“Mwokoaji anawajibika kuangalia iwapo aliyezama ana fahamu kwa kumpapasa au kutoa wito wa sauti kubaini iwapo anasikia,”anasema.

Anasema; Iwapo hatajibu ni ishara kuwa anaweza kuwa amepoteza fahamu, hivyo mwokoaji anapaswa kukagua upumuaji na mapigo ya moyo.

…Hilo hulifanya kwa kuangalia kama kifua kinacheza au kama kuna pumzi kwa kuweka sikio au vidole kifuani au shingoni.

Kama hapumui anasema mwokoaji amlaze chali kwenye eneo tambarare na anaweza kufungua njia ya hewa kwa kumwinamisha kichwa nyuma kidogo na kuinua kidevu kisha ampatie pumzi (CPR) hadi apumue au msaada wa afya ufike.

“Ikiwa mtu anaanza kupumua au kukohoa awekwe sehemu salama na kuendelea kuwa chini ya uangalizi hadi wahudumu wa afya wafike. Pia afunikwe ili kuzuia baridi kwa kutumia taulo, nguo kavu, blanketi au shuka,”anashauri.