Dar es Salaam. Wazazi wana jukumu kubwa katika ukuaji na malezi ya watoto wao. Malezi bora humsaidia mtoto kukua akiwa na maadili mema, kujiamini, na kuwa raia mwema katika jamii.
Hata hivyo, pamoja na nia njema ya kuwalea watoto vizuri, wazazi mara nyingi hufanya makosa ambayo huathiri ukuaji wa mtoto kimwili, kihisia na kiakili. Makosa kama haya yanaweza kuwa ya kawaida, lakini madhara yake mara nyingi huwa ya muda mrefu na yanaweza kuathiri maisha ya mtoto hata akiwa mtu mzima.
Katika makala haya, tutaangazia baadhi ya makosa makubwa matano ambayo wazazi hufanya katika malezi ya watoto wao. Moja ya makosa ya kawaida ni kulea watoto kwa misingi ya hofu badala ya maelewano.
Wazazi wengi huamini kuwa kwa kutumia hofu au vitisho, watoto watakuwa watiifu na wenye nidhamu. Wanaweza kutumia adhabu kali kama vile kupiga, kutukana, au kuwatishia watoto ili kuwafanya wafanye au waache jambo fulani. Ingawa mara nyingine watoto wanaweza kutii, msingi wa utiifu wao huwa ni woga na si kuelewa sababu ya kutii.
Hali hii hujenga hofu badala ya heshima na mtoto anaweza kukua akiwa na msongo wa mawazo, kutojiamini, au hata kuwa na hasira za ndani zinazoweza kujitokeza baadaye katika maisha yake. Makosa mengine hutokea pale wazazi wanaposhindwa kutenga muda wa kutosha wa kuwasikiliza.
Joyce Mtalemwa, mtaalamu wa saikolojia, anasema wazazi wengi wanalemazwa na maisha ya usasa yaliyojaa pilika nyingi. Anasema kutokana na hilo, wengi wao hujikuta wakitenga nafasi ndogo ya kuwa karibu na watoto wao jambo ambalo halina afya kwa familia.
Anachokisema Mtalemwa ni sahihi kabisa, wazazi wanaweza kuwa ‘bize’ na kazi, simu, au shughuli nyingine na kujikuta wakishindwa hata kumpa mtoto nafasi ya kueleza hisia, matatizo, au mafanikio yake.
Tukumbuke kuwa mtoto ambaye hasikilizwi anaweza kuhisi kuwa hathaminiwi au hapendwi na mzazi, jambo linaloweza kuathiri maendeleo yake ya kihisia.
Watoto wanapopata nafasi ya kuzungumza na kusikilizwa, hujenga ujasiri, kuelewa thamani yao na kuwa na mawasiliano bora katika maisha yao yote.
Pia, kuna tatizo la kulinganisha watoto na wengine. Wazazi wengine hujenga tabia ya kuwaambia watoto wao, “Angalia mtoto wa fulani, angalia alivyofaulu” au “Kwa nini huwezi kuwa kama ndugu yako?”
Ingawa lengo mara nyingi huwa ni kumhimiza mtoto ajitahidi zaidi, kulinganisha huleta madhara makubwa ya kisaikolojia. Mtoto huweza kujiona duni, asiye na thamani, au kujenga chuki dhidi ya yule anayelinganishwa naye.
Badala ya kumtia moyo, mtoto huweza kujenga hisia za kushindwa na kukosa motisha ya kuboresha mwenendo wake. Kila mtoto ni wa kipekee na anapaswa kulelewa kwa kutambua uwezo wake binafsi.
Makosa mengine hutokea pale ambapo wazazi huwapangia watoto wao maisha yao bila kuwashirikisha.
Wazazi wanaweza kuwa na matarajio makubwa kuhusu mustakabali wa mtoto wao, kama vile kumlazimisha achague taaluma fulani au kufanya kazi fulani kwa sababu ni ndoto ya mzazi, si ya mtoto.
Mtoto anapolazimishwa kufuata njia ambayo haina mvuto kwake, hupoteza dira na huweza kuwa na maisha yasiyo na furaha. Malezi bora yanapaswa kumwezesha mtoto kugundua vipaji vyake, kupenda anachofanya, na kuamua mwelekeo wa maisha yake kwa msaada wa mzazi na si kwa amri.
Baadhi ya wazazi hufanya makosa kwa kutoweka mipaka au sheria kwa watoto wao. Wazazi wanaweza kuwa wanyonge kiasi cha kuruhusu kila kitu anachotaka mtoto bila kumwekea mipaka au kumwajibisha.
Ingawa ni muhimu kumpa mtoto uhuru, uhuru usio na mipaka huweza kusababisha mtoto kukosa nidhamu, kutoheshimu mamlaka, na kutokuwa na uwezo wa kudhibiti tabia zake mwenyewe. Wazazi wanapaswa kuweka sheria zenye uwiano, kumfundisha mtoto umuhimu wa uwajibikaji, na kumwelekeza bila kumdhibiti kupita kiasi.
Kwa kumalizia, makosa ya wazazi kwenye malezi mara nyingi hutokea kwa sababu ya kutojua au kwa sababu ya kushindwa kusawazisha mapenzi kwa mtoto na nidhamu inayofaa.
Ni muhimu kwa wazazi kujitathmini, kujifunza, na kubadilika kadiri watoto wao wanavyokua. Malezi bora yanahitaji upendo, subira, mawasiliano, na uelewa wa hali ya mtoto mmoja mmoja. Mtoto anapolelewa kwa njia sahihi, huweza kufikia uwezo wake wa juu zaidi na kuwa mtu mwenye mchango chanya kwa jamii.