Mchungaji Hananja atoa neno kwa vijana

Kibaha. Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Jackson Hananja amewahimiza vijana nchini kuacha kulalamikia ugumu wa maisha na badala yake, watumie maarifa na ubunifu wao kujitafutia ajira halali.

Amesisitiza kuwa licha ya uhaba wa ajira rasmi unaoikabili nchi, fursa za kujiajiri bado zipo nyingi kama watajiongeza.

Akizungumza leo Jumapili Agosti 10, 2025 katika semina ya vijana yaliyofanyika katika Kanisa la PMC Kibaha, mkoani Pwani, Hananja amesema si kila mtu ataajiriwa, hivyo ni muhimu kwa vijana kujipanga na kuanzisha miradi inayoweza kuwapatia kipato.

“Maisha hayatatengenezwa na mtu mwingine. Vijana mnapaswa kuacha kukaa na kulalamika, badala yake muumize vichwa kutafuta suluhu. Kila kizazi kina changamoto zake na hiki kinahitaji akili na maarifa zaidi kuliko nguvu za misuli,” amesema mchungaji huyo.

Aidha, Hananja amewashauri vijana kuunda vikundi au taasisi za kijamii zitakazowawezesha kuaminika mbele ya Serikali na taasisi za kifedha ili kupata mitaji, vifaa au hata ardhi kwa ajili ya kilimo.

“Ukiwa na nguvu ya kundi na umoja, ni rahisi zaidi kupata msaada wa mitaji na ardhi kuliko ukiwa peke yako,” amesisitiza.

Askofu wa Kanisa la PMC, Gervas Masanja amesema lengo la semina hiyo ni kuwapa vijana mbinu na maarifa ya kufanya kazi ili kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Mmoja wa washiriki wa semina hiyo, Janeth Moses amesema elimu waliyoipata imempa msukumo mpya. “Nimejifunza kuwa hakuna kazi ndogo mradi iwe halali na inaleta kipato. Hii imenipa ujasiri wa kuanza kufikiria mradi wangu binafsi,” amesema.