USHINDI wa Mauritania dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati katika michuano ya CHAN 2024 umeibua matumaini mapya kwa kikosi cha Mourabitounes, huku mchezaji bora wa mechi hiyo, Ahmed Mokhtar Ahmed, akitamba juu ya ushindi huo.
Baada ya mechi mbili mfululizo bila kufunga dhidi ya Madagascar na Tanzania, presha ilionekana kuwa kubwa kwa washambuliaji wa Mauritania.
Lakini ndani ya dakika tisa tu hapo juzi, Jumamosi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Mokhtar alivunja ukame huo wa mabao.
Bao hilo pekee liliipa Mauritania ushindi wa bao 1-0 na pointi tatu muhimu.
“Nawapongeza wachezaji wenzangu na kocha baada ya ushindi dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati. Tumepata ushindi wetu wa kwanza kwenye CHAN, na tutajaribu kuonyesha kiwango bora zaidi katika mechi ijayo, Mungu akipenda,” alisema.
Kwa ushindi huo, Mauritania sasa wana pointi nne kwenye Kundi B, ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Tanzania yenye pointi tisa kileleni hatua inayowapa nafasi ya kuendelea kuwania kufuzu hatua ya robo fainali.
Katika mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi, Jumatano ya Agosti 13 Mauritania itacheza dhidi ya Burkina Faso ambayo nayo inasaka nafasi ya kutinga mtoano.