LICHA ya Taifa Stars kushinda mechi tatu mfululizo katika hatua ya makundi ya michuano ya CHAN 2024 na kufuzu robo fainali, kocha wa kikosi hicho, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amewataka wachezaji wake kuelekeza nguvu kwenye mechi ya mwisho ya hatua hiyo dhidi ya Afrika ya Kati ili kumaliza vinara wa Kundi B.
Stars ilianza kwa kishindo michuano hiyo kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso, Agosti 2, 2025, katika mechi ya ufunguzi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Mabao ya Abdul Suleiman ‘Sopu’ katika dakika ya 45+3 kupitia penalti na Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’ dakika ya 71 yalitosha kuleta mwanzo huo mzuri.
Agosti 6, 2025, Stars ilionyesha uimara wa kiufundi na kiakili kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mauritania, bao pekee likifungwa na Shomari Kapombe katika dakika ya 89 akimalizia pasi safi ya Iddy Selemani Nado na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu mapema.
Kisha Agosti 9, 2025, Stars ilikamilisha ushindi wa tatu mfululizo kwa kuichapa Madagascar mabao 2-1 kupitia mabao mawili ya Clement Mzize katika za dk13 na 20, huku bao la kufutia machozi la Madagascar likifungwa na Razafimahatana katika dk34.
Ushindi huo uliweka historia ya kufuzu robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano ya CHAN huku ikiwa na rekodi ya ushindi kwa asilimia mia moja.
Akizungumza na Mwanaspoti Morocco alisema: “Ninafurahia nidhamu na ari ya wachezaji wangu, lakini bado hatujamaliza kazi. Mechi dhidi ya Afrika ya Kati ni mtihani wa mwisho wa hatua ya makundi na tunahitaji kushinda ili kumaliza vinara wa kundi. Hii italeta morali kubwa kuelekea robo fainali.”
Kocha huyo aliongeza kuwa anaamini kikosi chake kinaweza kumudu changamoto kutoka kwa wapinzani wao, ambao wanajulikana kwa soka la nguvu na kasi na maandalizi yao yatajikita kwenye kuboresha uimara wa safu ya ulinzi na umakini wa safu ya ushambuliaji.
Stars imekuwa moja ya timu zinazofurahia sapoti kubwa ya mashabiki nyumbani, hali ambayo kocha amesema inawapa nguvu ya ziada.
“Ukiwa na mashabiki wanaokuamini, inakupa nguvu ya kupigana zaidi. Tunataka kutoa zawadi ya ushindi kwa Watanzania wote,” alisema.
Michuano ya CHAN mwaka huu imeandaliwa kwa mara ya kwanza na mataifa matatu; Kenya, Uganda na Tanzania, huku CAF ikipongeza maandalizi ya wenyeji, ikisisitiza viwango vya juu vya miundombinu na uendeshaji wa mashindano.
Kwa upande wa takwimu, Stars imefunga mabao matano na kuruhusu bao moja pekee katika mechi zote tatu za mwanzo, ikiongoza kundi kwa pointi tisa, na ikiwa miongoni mwa ngome bora kwenye mashindano haya.
Kikosi hicho pia kinajivunia wachezaji wachanga wenye kiu ya mafanikio, akiwemo Mzize mwenye umri wa miaka 21 ambaye ndiye kinara wa mabao wa timu, pamoja na kipa Yakoub Suleiman Ali ambaye ameokoa michomo muhimu na kulinda lango.
Hata hivyo, ‘Morocco’ amesisitiza kuwa changamoto kubwa ipo mbele: “Robo fainali inahitaji umakini zaidi, makosa madogo yanaweza kugharimu kila kitu. Tunataka kutumia mechi ya mwisho kama kipimo cha maandalizi yetu.”
Kama Stars itamaliza kinara wa Kundi B, katika robo fainali itacheza na timu iliyoshika nafasi ya pili Kundi A, ambalo kabla ya mechi za jana Jumapili lilikuwa likiongozwa na Kenya kwa pointi nne, kisha Morocco (pointi 3), sawa na DR Congo.