WAKATI presha ya kutafuta matokeo ikiikabili Taifa Stars, straika anayetajwa kuwa na thamani ya Sh2 bilioni, Clement Mzize aliibuka shujaa wa usiku wa Jumamosi, akiifanya Tanzania kuweka rekodi ya kibabe na kutinga robo fainali ya michuano ya CHAN 2024.
Mshambuliaji huyo alifunga mabao mawili ndani ya dakika 7 na kuiwezesha Tanzania kushinda 2-1 dhidi ya Madagascar, ushindi ulioipeleka robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Mzize alionekana mwenye furaha huku akionyesha kuwa na shauku ya kufika mbali zaidi katika mashindano hayo yanayofanyika Afrika Mashariki.
“Namshukuru Mungu kwa nafasi hii na kwa kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi. Ni jambo kubwa kuendelea mbele kwenye mashindano haya, na tunatarajia kwenda mbali zaidi,” alisema.
Madagascar ilionyesha upinzani mkali kwa kutumia nguvu na nidhamu ya kiufundi, lakini ubora wa Mzize katika kutafuta nafasi na kuzitumia ulifanya tofauti kubwa.
“Ilikuwa ngumu kutokana na uimara wa Madagascar, lakini tulijitahidi kufika langoni mwao na kufunga mabao mawili muhimu,” aliongeza.
Ushindi huo umeweka rekodi mpya kwa Tanzania, kwani hii ni mara ya kwanza inavuka hatua ya makundi kwenye CHAN.
Mzize alitambua ukubwa wa hatua hiyo, akisema: “Ni bahati kubwa kushiriki, na safari hii tumepita hatua ya makundi kwa mara ya kwanza. Tunastahili, na tunawashukuru mashabiki kwa kutupa nguvu ya kufika robo fainali.”
Mabao mawili ambayo Mzize alifunga dhidi ya Madagascar yamemfanya kuwa kinara wa mabao kwenye CHAN kwa idadi sawa ya mabao na Mkenya, Austin Odhiambo kabla ya mechi ya jana, ambapo majirani zetu hao walikuwa na kibarua kizito mbele ya Morocco.