Mradi wa maji wa Sh662 milioni wakomboa wananchi wa Meatu

Meatu. Wananchi wa kijiji cha Bulyashi kilichopo Kata ya Mwamishali wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu, wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.

Meneja wa Ruwasa wilaya ya Meatu,Mhadisi David Kaijage(kulia)akitoa maelezo kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2025,Ismail Ussi(wa pili kushoto)juu ya mtandao wa maji katika mradi wa maji katika kijiji cha Bulyashi wilayani humo.Picha na Samwel Mwanga

Hiyo ni baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), kuwajengea tanki la maji lenye ujazo wa lita 75,000.

Wananchi hao walikuwa wanatembea umbali wa kilomita 10 kutafuta maji huku ikiwachukua siku moja hadi mbili kuyapata.

Akizungumza leo Jumapili Agosti 10, 2025 baada ya kuwekwa kwa jiwe la msingi la Mradi wa Maji Bulyashi, mkazi wa kijiji hicho, Limi Maduhu amesema awali walikuwa wakitoka alfajiri kwenda kusaka maji ambayo pia walikuwa hawana uhakika wa usalama wake, kuyapata siku hiyohiyo.

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa 2025,Ismail Ussi(wa kwanza kulia)mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maji katika kijiji cha Bulyashi wilaya ya Meatu.Picha na Samwel Mwanga

“Tulikuwa tunatembea umbali mrefu sana kutafuta maji, hukohuko mnakaa foleni siku moja hadi mbili ndio urudi nyumbani, lakini kumalizika kwa mradi huu, tunashukuru sana hata ndoa zetu zitakuwa na amani sasa,” amesema.

Naye Emanuel Matulanya, mkazi wa Kijiji cha Bulyashi amesema ndoa nyingi zilivunjika kwa kuwa wake zao walikuwa wakichelewa kurudi na waume zao wakawa wanahisi vibaya kwamba wana wanaume wengine.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuleta fedha kwa ajili ya kutujengea mradi huu wa maji katika kijiji chetu cha Bulyashi na kwa sasa tuna vituo vya kuchotea maji vipatavyo 12, tumeshaondokana na adha ya maji,” amesema.

Meneja wa Ruwasa wilaya ya Meatu,Mhandisi David Kaijage(aliye kati)akisoma taarifa ya mradi wa maji katika kijiji cha Bulyashi wilaya humo kwa kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa 2025(hayupo pichani).Picha na Samwel Mwanga

Meneja wa Ruwasa, Wilaya ya Meatu, David Kaijage amesema mradi huo unatekelezwa na Kampuni Jovitech Engineering Company Ltd chini ya Ruwasa.

Amesema mpaka kukamilika kwake, umegharimu zaidi ya Sh662 milioni na utahudumia wakazi 2,725 wa kijiji hicho.

“Mradi huu umegharimu Sh662 milioni na umelenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi 2,725 wa kijiji cha Bulyashi,” amesema.

Naye mkimbiza Mwenge kitaifa mwaka 2025, Ismail Ussi amewataka wananchi hao kutunza miundombinu ya mradi huo ili utumike muda mrefu.

Mwenge wa Uhuru umekimbizwa katika Wilaya ya Meatu ambapo miradi sita yenye thamani ya Sh1.9 bilioni imefunguliwa, kuwekwa mawe ya msingi na kuzinduliwa.