Arusha. Hatimaye harakati za aliyekuwa Ofisa wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), Henry Kitambwa aliyemshtaki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupinga uamuzi wa kuridhia kufukuzwa kwake kazi kwa tuhuma za ubadhirifu, zimezaa matunda baada ya Mahakama ya Rufani kuridhia rufaa yake.
Uamuzi huo umetolewa Agosti 7, 2025 na jopo la majaji watatu, Ferdinand Lila, Dk Benhajj Shaaban Masoud na Ubena Agatho ambao walikubaliana na moja ya hoja za rufaa ya Kitambwa na kubatilisha mwenendo mzima wa kamati ya nidhamu iliyomjadili.
Kadhalika, mashauri yote yaliyomkabili Rais (mjibu rufaa wa kwanza) na yale ya Mahakama Kuu yaliyotokana na mashauri yaliyobatilishwa, yametangazwa kuwa batili na kufutwa.
Hivyo, amri ya kusimamishwa kazi kwa Kitambwa imefutwa.
Majaji hao wameelekeza kuwa iwapo mrufani huyo hajatimiza umri wa kustaafu, arejeshwe kazini na kulipwa mishahara yake.
“Ikiwa ameshafikia umri wa kustaafu, alipwe mishahara kuanzia tarehe aliyosimamishwa kazi hadi alipostaafu, pamoja na marupurupu ya kustaafu kwa mujibu wa sheria,” imeelekeza hukumu hiyo.
Katika rufaa hiyo ya madai namba 460/2022, Kitambwa alikuwa amewashtaki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Desemba 19, 2019.
Mahakama ya Rufani, katika rufaa ya awali ya Kitambwa iliyoamuliwa na jopo la majaji watatu, Mwanaisha Kwariko, Zephrine Galeba na Patricia Fikirini, ilitupilia mbali rufaa hiyo baada ya kubaini dosari.
Dosari iliyobainika kabla ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo, ilikuwa kukosekana kwa nyaraka muhimu za Mahakama, ikiwamo barua ya Msajili kumjulisha Kitambwa kuhusu kukamilika kwa nyaraka za kumbukumbu ya rufaa.
Nyaraka hizo hujumuisha mwenendo wa kesi, hukumu au uamuzi unaopigiwa rufaa, vielelezo na nyaraka nyingine zinazotakiwa kuambatanishwa na rufaa, ambazo huandaliwa na Mahakama au mrufani mwenyewe.
Hii ilikuwa ni mara ya tatu kwa Kitambwa kuangukia pua katika jitihada zake za kupinga kufukuzwa kazi, rufaa mbili katika ngazi za kiutumishi na kiutawala na nyingine mbili katika mhimili wa Mahakama.
Kitambwa, aliyekuwa amehamishiwa kwa muda kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwenda Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, aliachishwa kazi Februari 20, 2017 na kamati ya nidhamu, akituhumiwa kujipatia Sh123.3 milioni kwa njia za udanganyifu.
Baada ya kufukuzwa kazi, alikata rufaa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), lakini Oktoba 25, 2017, tume hiyo ilitupilia mbali rufaa yake na kuunga mkono uamuzi wa kamati ya nidhamu. Kitambwa aliamua kukata rufaa kwa Rais, akipinga uamuzi wa tume hiyo, lakini Desemba 26, 2017 (na kuwasilishwa kwake Januari 11, 2018), Rais aliridhia uamuzi huo.
Baada ya kushindwa kwa njia za kiutawala, Kitambwa aliamua kufungua shauri Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Rais.
Hata hivyo, Desemba 19, 2019, Jaji Joacquine De Mello alitupilia mbali shauri hilo, akisema uamuzi wa Rais ulikuwa halali na ulizingatia sheria.
Hata hivyo, Kitambwa hakuridhika, alikata rufaa Mahakama ya Rufani ambayo ni mahakama ya juu zaidi yenye uamuzi wa mwisho dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
Miongoni mwa hoja zake, Kitambwa alidai kuwa uamuzi wa Rais ulikuwa batili kwa madai kwamba ulienda kinyume na sheria, hususan Kanuni ya 47(10) ya Kanuni za Utumishi wa Umma, Tangazo la Serikali Na. 168 la mwaka 2003.
Katika rufaa ya sasa, Kitambwa alipinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliotupilia mbali maombi yake ya kutengua uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Desemba 26, 2016, uliobariki kufukuzwa kwake kazi.
Mrufani aliwasilisha sababu nane za rufaa, akidai kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu na makosa ya kisheria katika mchakato wa kufukuzwa kwake kazi.
Kitambwa alisema miongoni mwa madai yake ni mjibu tufaa wa tatu hakuwa na mamlaka ya kinidhamu, uchunguzi uliofanywa dhidi yake ulifanyika nje ya muda kinyume na kanuni na kwamba, alinyimwa haki ya kujitetea kwa kukosa nyaraka, mashtaka na vielelezo vya maandishi vilivyotumika kumtia hatiani. Pia alilalamika kwamba Mahakama Kuu ilishindwa kumpa nafuu aliyoomba.
Kabla ya kufukuzwa kazi, Kitambwa alikuwa Mwanasheria wa Serikali Daraja la Kwanza, akiajiriwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na baadaye kuhamishiwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), kama Mkuu wa kitengo cha huduma za sheria.
Katika rufaa yake, aliongozwa na Wakili Mpaya Kamara na wenzake, huku upande wa wajibu rufaa ukiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Deodatus Nyoni na timu yake.
Majaji hao wamesema katika kuamua rufaa na baada ya kuchunguza sababu za kukata rufaa na kwa kuzingatia mawasilisho ya pande zote, wanaona ni vema kuanza na msingi wa pili wa rufaa kuhusu ukomo wa muda na inaweza kuwa bora kwa sababu wakiipata ina uhalali inaweza kuondoa rufaa yote.
Sababu hiyo ni kuwa uchunguzi ulianza Januari 6, 2017 ikiwa muda wa uchunguzi kwa mujibu wa kanuni ya 47(10) ya Kanuni za Utumishi wa Umma ukiwa umepita hivyo chochote kinachofanyika nje ya muda kinakuwa batili.
Wakili Nyoni alikubali kwamba uchunguzi ulianza nje ya wakati na kuwa mrufani alipewa notisi ya shitala Oktoba 17,2016 na kusikilizwa kulianza Januari 6,2017 hivyo kukiri kuwa uchunguzi huo ulikuwa nje ya muda kwa siku 22, kwani siku 60 kwa mujibu wa sheria ziliisha Desemba 15,2016 na kueleza ukiukwaji huo unatibika.
Jaji Agatho amesema rekodi ya rufaa zipo wazi kwenye ukurasa wa 89 kwamba walalamikiwa walikanusha shtaka la uchunguzi kuanza nje ya muda na kusema kuwa uamuzi wa mjibu rufaa wa tatu ulikuwa halali na ndani ya muda uliowekwa kwa mujibu wa sheria husika.
Amesema katika kuchunguza msingi uliotajwa, na wakati wa kuiondoa watazingatia kanuni ya 62(3) ya PSR na kuamua uhusiano wake ikiwa upo na kanuni ya 47(10) ya Kanuni hizo hizo.
Amesema wana maoni yanayozingatiwa kuwa uchunguzi ulifanyika nje ya wakati na mrufani hakujulishwa uchunguzi ulipoanzishwa.
“Hakuna ushahidi wowote wa kuonyesha ni lini kamati hiyo iliteuliwa kwa tarehe yoyote ya awali zaidi ya Desemba 16, 2016. Zaidi ya hayo, notisi ya uchunguzi iliwasilishwa kwa mrufani kupitia taarifa ya shtaka Desemba 30, 2016 wakati kikomo cha muda wa siku 60 kilichowekwa kwa ajili ya kuanza kwa uchunguzi kilipokwisha,”
“Mbaya zaidi siku ilipotaka mrufani afike mbele yao nayo ilikuwa imepitwa na wakati, kinyume chake, ushahidi pekee unaoonyesha kwamba uchunguzi ulianza Desemba 13,2016 ni barua ya kuongeza muda ambayo haikuwasilishwa kwa mrufani,” amesema Jaji.
Jaji Agatho amesema wakati wa kusikilizwa kwa Wakili Mkuu wa Serikali alikubali kwamba uchunguzi ulifanyika nje ya wakati na kuwa ni maoni yao kuanza uchunguzi nje ya muda uliopangwa, kamati ya nidhamu ilikiuka sheria na mwenendo mzima ulikuwa batili.
Amesema kukiukwa huko ina maana kwamba mjibu rufaa wa tatu alitekeleza majukumu yake bila mamlaka, akinukuu maamuzi mbalimbali ya mahakama hiyo ambayo yanaeleza sheria ya ukomo wa muda inalenga kuhakikisha haki za wadai zinaamuliwa kwa wakati.
“Katika sheria, matokeo ya kufanya jambo lolote nje ya wakati ni kulifanya kuwa ubatili kwa kukosa mamlaka. Baada ya kuchunguza rekodi ya rufaa na sheria, tunaona kwamba uchunguzi lazima uanze kabla ya kuisha kwa siku 60 kama ilivyoainishwa chini ya kanuni ya 47 (10) ya PSR,” amesema.