Mzize aendeleza rekodi michuano ya CAF

MABAO mawili aliyofunga dakika ya 13 na 20 yaliyoiwezesha Taifa Stars kutinga robo fainali ya michuano ya CHAN 2024, Clement Mzize kuendeleza rekodi tangu katika michuano inayoendeshwa na CAF.

Mzize aliiwezesha Stars kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Madagascar ikiwa ni wa tatu mfululizo wa Kundi B na kutinga robo fainali kwa mara ya kwanza ikifikisha pointi tisa.

Hii ni mara ya pili kwa Mzize kufunga mabao muhimu katika michuano ya CAF, baada ya misimu miwili iliyopita kufunga pia mabao mawili katika mechi mbili tofauti, wakati Yanga ikitinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 25, tangu ilipocheza hatua hiyo mwaka 1998.

Mabao hayo ya Mzize pia yalivunja mwiko wa Yanga kushindwa kutamba mbele ya El Merrikh ya Sudan, kwani iliwafunga nje ndani kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0 na kutinga makundi kabla ya kutolewa robo fainali na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Mzize alifunga bao la pili jijini Kigali wakati Yanga ikishinda 2-0, kisha kuongeza jingine la pekee jijini Dar es Salaam na kutinga makundi, kama alivyofanya usiku wa jana lakini safari hii akiwa na timu ya taifa kwa kuivusha Stars hadi robo fainali ya CHAN 2024.

Kabla ya hapo, Stars ilikuwa haijawahi kuvuka hatua ya makundi ya fainali zote cha CAF, ikiwa Afcon ilizoshiriki mara tatu 1980, 2019 na 2023 pamoja na mbili za CHAN 2009 na 2020.

Ushindi wa jana usiku ulikuwa ni wa tatu mfululizo kwa Stars na kuongoza Kundi B na kuwa ya kwanza kwenda robo fainali.

Mechi ya kwanza Stars ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso kabla ya kuilaza Mauritania kwa bao la dakika za jioni la Shomari Kapombe na jana usiku ikatamba 2-1 yote akifunga Mzize.

Stars imecheza kwa nidhamu kubwa ikiheshimu Madagascar iliyokuwa na kasi kwa dakika 30 za kwanza, ikichez akwa utulivu kwa pasi sahihi zilizozaa matunda na kuisaidia timu hiyo hadi mapumziko ikiongoza 2-1.

Bao la Madagascar lilifungwa dakika ya 34 na Nantenaina Mika Razafimahatana, ambaye hakumaliza mchezo baada ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Fenohasina Gilles Razafimaro.

Baada ya Madagascar kupata bao la kufutia machozi, Stars iliongeza umakini eneo la ulinzi na kupambana kutafuta bao lakini uimara wa wapinzani uliwazuia hadi filimbi ya mapumziko.

Kipindi cha pili timu zote ziliingia kwa kasi, huku kila timu ikitafuta bao, Stars ikisaka la tatu na Madagascar ikitafuta la kusawazisha.

Umakini wa safu ya ulinzi ulikuwa na faida zaidi kwa Stars, ambayo imetumia dakika 90 kuvuna pointi tatu na kuongoza kundi B, huku Madagascar ikisaliwa na pointi moja iliyopata kutokana na suluhu dhidi ya Mauritania.

Stars mapema dakika 19 Abdurazak Hamza alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Shekhan Khamis ambaye pia hakumaliza dakika 90 kwani alitolewa kumpisha Nassor Saadun, naye Idd Seleman ‘Nado’ alitolewa kumpisha Pascal Msindo.

Stars imebakiza mechi moja ya kukamilisha ratiba dhidi ya Afrika ya Kati itakayopigwa Jumamosi ijayo ili kujua kama itamaliza kileleni au nafasi ya pili, ili kujua itacheza na timu ipi kutoka kundi A katika robo fainali.

Kikosi cha Stars kilichoanza, Yakoub Suleiman, Ibrahim Hamad, Dickson Job, Abdurazak Hamza, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Idd Seleman, Feisal Salum, Abdul Suleiman ‘Sopu’, Mudathir Yahya na Clement Mzize.

Kikosi cha Madagascar kilichoanza, Ramandimbosoa Lalain’arinjaka, Nantenaina Elysee, Hajatiana Ratsimbazafy, Nantenaina Andy Rakotondrajoa, Nomena Rafanomezantsoa, Nantenaina Mika, Jean Luc Ranaivoson, Bono Stephanot, Toky Rakotondraibe, Rado Niaina na Mamiso Rakotoson.