NADES-FORMATION YAWAELIMISHA WAKULIMA WA DODOMA KUHUSU KILIMO MSETO na UTUNZAJI WA MAZINGIRA


 SHIRIKA lisilo la kiserikali la INADES-Formation Tanzania limetumia Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima Nanenane Kanda ya Kati yaliyofanyika kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma kutoa mafunzo mbalimbali kwa wakulima wa wilaya za Chemba na Kondoa kuhusu kilimo mseto na utunzaji wa mazingira.

Afisa Mradi wa Kilimo Mseto kutoka shirika hilo, Paul Chugu, alisema mafunzo hayo yalitolewa kwa wadau waliotembelea banda la INADES-Formation Tanzania

wakiwemo wakulima kutoka vijiji vya miradi vya Itundwi, Filimo, Bambare na Kwayondu, ili kuwawezesha kuongeza ufanisi katika kilimo endelevu na kukabiliana na athari hasi za mabadiliko ya tabianchi.

Miongoni mwa masuala waliyofundishwa ni umuhimu wa kuthamini na kuzalisha mbegu za asili, kutumia fursa ya uzalishaji iliyotolewa na TOSCI, pamoja na uuzaji wa mbegu hizo baada ya kuidhinishwa. Pia walifundishwa kuhusu ufugaji wa samaki, mbuzi, kuku na ng’ombe, teknolojia za umwagiliaji kwa matone, utengenezaji wa mboji, na aina ya miti inayofaa kwa kilimo mseto.

Chugu alieleza kuwa kilimo mseto kinamwezesha mkulima kupata mapato kutoka vyanzo mbalimbali kama mbao, matunda, karanga, kuni, asali na mazao ya shambani kutoka kwenye kipande kimoja cha ardhi, sambamba na kulinda mazingira na kuongeza tija ya muda mrefu.

Wakulima walioshiriki maonesho hayo walisema kilimo mseto kimewasaidia kulinda miti shambani, kuzuia mmomonyoko wa udongo, kupunguza nguvu ya upepo, kuhifadhi unyevu na kutoa kivuli kwa mimea na wanyama. 

Kasimu Njou, mkulima kutoka kijiji cha mradi, alisema kupitia kilimo mseto, wakulima wameweza kujiinua kiuchumi kwa kuuza matunda, mbogamboga na mazao mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa INADES-Formation Tanzania, Mbarwa Kivuyo, alisema shirika hilo pia lilitumia maonesho hayo kuhamasisha ustawi wa mnyama kazi punda kwa kauli mbiu “Pakia kwa Kujali”. Aidha, alibainisha mpango wa kujenga kituo cha mafunzo kwa wakulima katika wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma, ili mafunzo hayo yatolewe muda wote.

Kivuyo alitoa wito kwa wadau wa maendeleo kushirikiana nao kuongeza fursa za mafunzo kwa wakulima, akisisitiza kuwa “Wakulima wadogo ndio wanaolisha taifa, hivyo ni muhimu wapewe mafunzo ya kilimo mseto ili waongeze tija na kulinda mazingira.”

Mfanyakazi wa Kitengo cha Mafunzo kwa Masafa cha INADES-Formation Tanzania, akitoa maelezo kwa wadau mbalimbali pamoja na mfadhiri wa mradi wa kilimo mseto, Vi Agroforestry, kuhusu masuala ya kilimo ikiwemo kilimo mseto, katika banda la shirika hilo wakati wa Maonesho ya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma