Nishati safi ya kupikia: Suluhisho la afya na mazingira endelevu

Dar es Salaam. Matumizi ya nishati isiyosafi kupikia hasa kuni na mkaa yanaleta madhara ya kiafya, kijamii, kiuchumi na kimazingira.

Tanzania na Dunia zimeweka mikakati kukabiliana na haya kwa kupunguza au kuacha kabisa matumizi haya yasio salama kwa sasa na vizazi vijavyo.

Lengo namba saba la maendeleo endelevu ya dunia (SDG 7) linalenga kuhakikisha watu wote duniani wanapata nishati ya kutosha, salama, nafuu na isiyoathiri mazingira, hasa kwa kutumia vyanzo vya nishati vinavyoweza kurejeshwa kama vile jua, upepo na maji.

Malengo haya (jumla yapo 17) yaliyoanzishwa mwaka 2015 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (na kusainiwa na nchi wanachama ikiwemo Tanzania) yanayolengwa kufikiwa ifikapo mwaka 2030.

Nishati safi na nishati safi ya kupikia sio lengo pekee linaloguswa bali SDG 3 (afya njema), SDG 5 (usawa wa kijinsia) na SDG 13 (hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi).

Pia, ni utekelezaji wa mchango wa kitaifa uliokusudiwa kukabili mabadiliko ya tabianchi (NDCs) chini ya Mkataba wa Paris kwenye makubaliano ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) , na kuipa nafasi nchi ya kuwa kiongozi wa kanda ya Afrika katika mageuzi ya mifumo ya nishati.

Ndani ya nchi kwenye suala la nishati, Tanzania imefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha hili, mfano kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwenye takwimu za mara kwa mara (High frequency data) inaonyesha mwaka 2015 vyanzo vya umeme vinavyotokana na Nishati safi vilichangia asilimia 37 pekee.

Lakini hadi Machi 2025 vya vyanzo vya nishati safi vilichangia karibu asilimia 70 ya nishati ya umeme.

Nishati sio kwenye umeme pekee, bali pia kwenye matumizi mengine ikiwemo kupikia. Kwenye hili nchi imefanya mambo mbalimbali ikiwapo kuwa kinara kwa kuongoza nchi za Afrika kwenye matumizi ya nishati mpya.

Mfano Desemba 2023 kwenye mkutano wa kidunia wa mabadiliko ya tabianchi (COP28) uliofanyika huko Dubai – Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Rais Samia Suluhu Hassan aliongoza mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na ulifanyika uzinduzi wa Mpango wa Kuwawezesha Wanawake wa Afrika katika Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (AWCCSP).

Kwa ngazi ya nchi Mei 2024 Rais alizindua Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024 -2034) uliolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania nchini zinatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.

Mkakati huo mahususi ulikuja kutokana na uhalisia kwamba Mpango wa Utekelezaji wa Nishati ya Kupikia wa Mwaka 2022 ulisema takriban asilimia 82 ya nishati ya msingi inayotumika nchini inatokana na vyanzo vya kibaomasi (kuni,mkaa…).

Pia iliongeza kwa matumizi ya kupikia, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 90 ya kaya nchini hutegemea kuni na mkaa kama chanzo chao kikuu cha nishati ya kupikia ambapo kuni zinachangia asilimia 63.5 na mkaa asilimia 26.2.

Mkakati huo unasema matumizi ya nishati chafu ya kupikia, hususan kuni na mkaa, yana madhara makubwa kwa afya, mazingira, uchumi, elimu na maisha ya kijamii.

“Kiafya, moshi unaotokana na nishati hizi hubeba gesi zenye sumu na chembechembe ndogo hatari zinazoweza kudhoofisha mfumo wa upumuaji na kusababisha magonjwa sugu kama kikohozi, nimonia, kifua kikuu, pumu na saratani ya mapafu” unanukuu mkakati.

Sumu hizi pia husababisha matatizo ya mimba, kuzaliwa kabla ya wakati au watoto wenye matatizo ya kiafya.

Magonjwa mengine yanayohusiana na moshi ni maradhi ya moyo, macho, shinikizo la damu na kupooza. Watoto chini ya miaka mitano na wanawake wanaokaa muda mrefu jikoni ndio waathirika wakuu.

Wengi pia hubeba kuni kichwani au mgongoni, hali inayowaathiri uti wa mgongo, kichwa na miguu. Takriban watu 33,000 hufariki kila mwaka nchini kutokana na magonjwa ya mfumo wa hewa yanayosababishwa na uchafuzi wa hewa majumbani.

Kimazingira, uvunaji wa kuni na uchomaji wa mkaa husababisha uharibifu mkubwa wa misitu. Kila mwaka, takribani hekta 469,420 za misitu huharibiwa, jambo linalochochea ukame na kuathiri ikolojia. Hali hii imechangia takriban asilimia 16 ya eneo la nchi tayari kubadilika na kuwa jangwa.

Katika nyanja ya kijamii, kutafuta kuni ni jukumu linalowalazimu wanawake na watoto kusafiri umbali mrefu, jambo linalowaweka kwenye hatari ya ukatili wa kijinsia kama kubakwa, kushambuliwa na wanyamapori au mateso ya kifamilia kutokana na kurejea nyumbani kuchelewa. Hali hii pia huondoa fursa ya kushiriki kwenye shughuli za kijamii na kisiasa.

Jambo hili linaathiri uchumi pia kwani kutafuta kuni huchukua wastani wa saa sita kila siku, muda ambao ungeweza kutumika katika shughuli za uzalishaji mali, elimu au ajira binafsi.

Kwenye elimu watoto na wanawake hupoteza nafasi ya masomo kwa sababu ya muda mwingi unaotumika kutafuta kuni, hali inayopunguza maendeleo yao kielimu na kiuchumi.

Mkakati unataja bayana kufanikisha kuwafikia Watanzania wengi kutumia nishati safi lazima wadau washirikiane.  Sekta binafsi ina jukumu la kushirikiana na Serikali kuhakikisha upatikanaji wa uhakika na endelevu wa nishati safi ya kupikia, kushiriki katika uhamasishaji na kuongeza uelewa wa umma kuhusu nishati safi ya kupikia.

Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kutumia kaulimbiu ya ‘Kuliwezesha Taifa’ tunashirikia kwenye kutoa elimu, kuandaa na kutekeleza programu zitakazowawezesha watu wenye kipato cha chini kumudu kupata suluhisho za nishati safi ya kupikia, kushirikiana na Serikali kubaini sera, sheria, kanuni na miongozo inayokwamisha jitihada kwenye hili.

Vilevile kuhakikisha mtandao wa usambazaji wa nishati safi ya kupikia, vifaa na majiko unafikia maeneo yote nchini na kuanzisha fursa za ajira katika sekta ya nishati safi ya kupikia.

Mwanzoni mwa Septemba 2025 MCL itafanya Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia litakalobeba mada isemayo: “Nishati Safi ya Kupikia: Okoa Maisha, Linda Mazingira”, tukio litakalokusanya pamoja wadau kujadili, kubadilishana uzoefu na kusukuma mbele ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini.

Kuelekea mjadala huu Agosti 11, 2025 MCL imeandaa majadiliano ya mtandaoni (Mwananchi Space) kwenye mtandao wa X tukijadili mada ya “Nini kifanyike, Watanzania watumie nishati safi ya kupikia kulinda mazingira na Afya zao”.

Kwenye jukwaa hilo kutajadiliwa kwa kina kuhusu ubunifu, sera, na watu wanaoendesha mageuzi kwenye nishati safi  na kwa nini lazima mabadiliko yafanyike sasa.

Vilevile itaendelea kutoa  machapisho maalumu baada ya mijadala hiyo hadi siku ya kongamano na baada ya hapo kwa njia ya makala za video, picha na simulizi kutoka kona mbalimbali za Tanzania  kupitia magazeti na majukwaa ya mtandaoni.

Kupitia makala hizo utafanyika uchambuzi wa kina kuhusu masuala ya afya, mazingira, usawa wa kijinsia, ubunifu wa vijana, sera, sheria, kanunu na kujadili suluhisho zinazobadilisha maisha ya kila Mtanzania.

Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.