NM-AIST yasisitiza ubunifu wa teknolojia

Arusha. Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Profesa Maulilio Kipanyula amesema taasisi hiyo imejikita kuunganisha taaluma na mahitaji halisi ya jamii.

Amesema hilo linafanyika kwa kutumia  ubunifu wa kiteknolojia ambao ni  nyenzo muhimu ya kuzalisha ajira endelevu kwa vijana na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Akizungumza leo Jumapili, Agosti 10, 2025, katika hafla ya kuwaonesha wafanyakazi wa taasisi hiyo tuzo ya ushindi wa kwanza waliopata katika kipengele cha taasisi za elimu ya juu kwenye maonyesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini, Profesa Kipanyula amesema taasisi hiyo imejikita kuunganisha taaluma na mahitaji halisi ya jamii.

“Teknolojia na ubunifu si chanzo tu cha ajira, bali pia ni nguzo ya kufanikisha dira ya Taifa ya kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa na ubunifu wa ndani,” amesema Profesa Kipanyula.

Ameongeza kuwa changamoto zilizopo kwenye jamii zinapaswa kuonekana kama fursa kwa vijana kuibua mawazo mapya ya kiteknolojia, kufanya tafiti na kuzalisha suluhisho linaloweza kuuzwa na kuwa chanzo cha kipato.

Profesa Kipanyula amesema NM-AIST, kwa kushirikiana na wafanyakazi wake, imeanzisha programu maalumu za kukuza ubunifu wa vijana ili miradi yao iweze kugeuzwa biashara endelevu.

Aidha, amebainisha kuwa taasisi hiyo imefanikisha tafiti na uvumbuzi wenye manufaa makubwa, ikiwamo chanjo ya samaki aina ya sato dhidi ya magonjwa, teknolojia ya kuzalisha mbolea kutoka taka za nyumbani na unga wa lishe wa kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.

“Tunawaelekeza wanafunzi wetu kufanya tafiti zinazojibu matatizo ya jamii, badala ya tafiti zinazolenga kuchapishwa tu kwenye majarida. Lengo ni kuhakikisha kila mradi wa utafiti una soko tayari, mteja wa kwanza akiwa yule anayekabiliana moja kwa moja na changamoto husika,” amesema Profesa Kipanyula.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa NM-AIST, Alkaeli Maro amesema tafiti zenye tija ni zile zinazopata uendelezaji na msaada wa wadau ili zifikie malengo yaliyokusudiwa.

“Ziko tafiti nyingi zimebaki kwenye makabrasha, hivyo natumia nafasi hii kuwaalika wadau wa sekta mbalimbali kujitokeza kuendeleza tafiti zinazohusiana na sekta zao ili kupata majawabu ya changamoto,” amesema Maro.