NMB yatoa mikopo ya zaidi ya Trilioni moja kwa wakulima na wafugaji nchini

Na Pamela Mollel,Arusha 

Benki ya NMB imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni moja mwaka 2025, kwa ajili ya kuwawezesha wakulima na wafugaji nchini kutekeleza miradi yao ya kilimo na mifugo.

Akizungumza katika Maonyesho ya Wakulima ya Nane Nane Kanda ya Kaskazini, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Praygod Godwin, alisema benki hiyo imeendelea kuwa mshirika muhimu wa sekta ya kilimo kwa kutoa mikopo nafuu na huduma jumuishi hasa masuluhisho ya kifedha zinazolenga kuongeza tija na kuboresha maisha ya wakulima na wafugaji.

“Lengo letu ni kuwawezesha wakulima na wafugaji sio tu kupata mitaji ya kuendesha shughuli zao, bali pia kuwapa elimu ya kifedha, bima ya kilimo na mifugo na huduma bora za kibenki ili waweze kustawi kiuchumi na kudumu kwenye biashara zao,” alisema Godwin.

Alisema mikopo hiyo inatolewa katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo na ufugaji kuanzia ununuzi wa pembejeo kama mbolea, mbegu na madawa ya kilimo, vifaa na mashine za kulimia na kuvuna, hadi miundombinu ya kuhifadhia na kuchakata mazao.

“Na hii Iko kwenye mpango wa “lipa baada ya kuvuna” ambayo imekuwa mkombozi kwa wakulima na wafugaji, kwani unawapa nafasi ya kurejesha mikopo baada ya kuuza mazao yao au mifugo, hivyo kuondoa mzigo wa malipo wakati wa msimu wa uzalishaji.

Amesema mbali na mikopo pia NMB imeendelea kutoa semina na mafunzo ya elimu ya fedha Kupitia NMB foundation ili kuwasaidia wakulima na wafugaji kupanga matumizi, kusimamia mapato na kuendeleza biashara zao.

Mbali na hilo pia tuna huduma za bima ambazo zimekuwa kinga ya hasara wakati wa majanga kama ukame, mafuriko au magonjwa ya mimea na mifugo.

Amesema hadi sasa wamefanikiwa kufikia zaidi ya wakulima na wafugaji milioni 2.4 katika vijiji 2000 nchini.

“Kikubwa wananchi waendelee kuiamini benki ya NMB kuwa ndio mkombozi wao wa changamoto zozote za kifedha na wahudhurie katika matawi yetu zaidi ya 240 nchi nzima kupata elimu na fursa tulizonazo kwa ajili yao” amesema 

Akifunga maonyesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amewataka wakulima nchini kuhakikisha wanaegemea katika matumizi ya teknolojia kuendeleza shughuli zao za kilimo kwa ajili ya kupata tija zaidi.

“Kilimo cha kizamani cha kulima na jembe la mkono na kupalilia kisha baadae kuvuna kwa mikono imepitwa na wakati, na huwezi kupata tija, nendeni kwenye taasisi za utafiti na bunifu kupata teknolojia za kuendesha kilimo chenu” amesema.

Mbali na hilo amewataka maafisa kilimo kuhakikisha wanawapa wakulima na wafugaji elimu ya kilimo na ufugaji wa kisasa ili waweze kunufaika zaidi.

“Pia muwaonyeshe wananchi wetu fursa za kifedha na bima zinazotolewa na taasisi zetu za kifedha ili wazijue na wazitumie kukuza kazi zao na uchumi kwa ujumla”.

 Neema Mollel, mkulima wa mbogamboga kutoka Wilaya ya Arumeru, amesema kuwa kupitia mkopo wa NMB mwaka 2023 amefanikiwa kununua mfumo wa kisasa wa umwagiliaji na kuongeza uzalishaji wake mara tatu.

“Nilipata mkopo wa mashine wenye riba nafuu, na sasa nimeunganisha katika kisima changu nyumbani na nalima mahindi na maharage na nimeongeza tija ya kilimo changu mara tatu zaidi ya mwanzo nilivyokuwa nategemea mvua pekee”