Sababu kifo cha Job Ndugai

Dar es Salaam. Katibu wa Bunge la Tanzania, Baraka Leonard amesema Spika mstaafu wa Bunge, Job Ndugai amefariki dunia kutokana na shinikizo la damu kushuka, iliyosababishwa na maambukizi makali kwenye mfumo wa hewa.

Ndugai alifariki dunia saa 9 alasiri ya Agosti 6, 2025 jijini Dodoma baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai enzi za uhai wake.

Leonard ameyasema hayo jijini Dodoma leo Jumapili, Agosti 10, 2025 aliposoma wasifu wa marehemu Ndugai katika viwanja vya Bunge ilipofanyika shughuli ya kitaifa ya kumuaga kabla ya kwenda kuzikwa kijijini kwao Kongwa jijini Dodoma.

 “Kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, alifariki kutokana na shinikizo la damu kushuka sana, iliyosababishwa na maambukizi makali kwenye mfumo wa hewa,” amesema.

Amesema Ndugai ameacha mke, watoto na wajukuu. Waombolezaji wengi wamejitokeza kushiriki safari hiyo ya mwisho ya Ndugai akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete.

Wengine ni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko na Jaji Mkuu, George Masaju.

Pia wapo, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Stephen Wasira na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Endelea kufuatilia Mwananchi