MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta atakuwa akilipwa kibosi huko Ufaransa kufuatia kujiunga na Le Havre AC inayoshiriki Ligue 1, akiwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kuvaa jezi ya klabu hiyo kongwe.
Kwa mujibu wa makadirio ya mishahara ndani ya Ligue 1, wachezaji wa timu za kiwango cha kati kama Le Havre hupokea kati ya Euro 50,000 hadi 150,000 kwa mwezi, takriban zaidi ya Sh140 milioni hadi Sh420 milioni.
Kwa Samatta ambaye ana historia ya kuzichezea klabu kubwa Afrika na Ulaya, kiwango chake kinatazamiwa kuwa kikubwa zaidi kutokana na uzoefu na hadhi yake kimataifa.
Mshahara huo utakuwa ni sehemu ya mapato yake, kwani mkataba wake pia unadaiwa kuhusisha bonasi ya mabao ambayo atakuwa akifunga, ushindi wa mechi na mafanikio ya timu.
Vyanzo vya ndani vya soka la Ufaransa vinabainisha kuwa nyota wa safu ya ushambuliaji kama Samatta huongezewa kati ya Euro 5,000 hadi 10,000 (takriban Sh14 milioni hadi Sh28 milioni) kwa kila bao analofunga au kuchangia kwa kiwango kikubwa ushindi wa timu.
Endapo Le Havre itafanikisha lengo la kusalia Ligue 1 msimu ujao au kushiriki michuano ya Ulaya, Samatta na wenzake wanaweza kulipwa bonasi ya msimu inayokadiriwa kufikia Euro 50,000 hadi 100,000 (takriban Sh140 milioni hadi Sh280 milioni).
Hii ni mbali na marupurupu ya kujiunga (signing bonus) ambayo kwa wachezaji wenye majina makubwa hufikia hadi euro 250,000 (takriban Sh700 milioni).
Samatta, mwenye umri wa miaka 32, amejiunga na klabu hiyo ya Ufaransa akiwa na mafanikio ya kutosha ikiwa ni pamoja na bingwa mara nne wa Ligi Kuu ya DR Congo na TP Mazembe, mshindi wa Ligi ya Mabingwa Afrika 2015 na mfungaji bora wa michuano hiyo, bingwa wa Ubelgiji na KR Genk, na bingwa wa Ligi Kuu ya Ugiriki na PAOK.
Katika uchezaji wake wa soka la kulipwa pia ameichezea Aston Villa ya England, Fenerbahce ya Uturuki na Royal Antwerp na KR Genk za Ubelgiji.