WAKATI Simba ikiendelea na maandalizi yake ya msimu ujao huko Ismailia, Misri, maisha ya mastaa wapya yameanza kuibua vaibu kambini, huku kila mmoja akijifua kwa ajili ya kuanza mapema kabisa kulishawishi benchi la ufundi la timu hiyo.
Simba inayojifua kwa ajili ya mashindano ya msimu ujao Bara na Afrika, imejifungia katika eneo tulivu ikifanya mambo yake, huku mambo mbalimbali yakihanikiza viunga hivyo katika taifa la Kiafrika lililopo Kaskazini mwa bara hili.
Haka hivyo, ni katika maandalizi hayo ambapo kocha wa kikosi hicho, Fadlu Davids ameonyesha kuvutiwa na mwenendo wa wachezaji wapya akiwemo Jonathan Sowah aliyesajiliwa kutoka Singida Black Stars na Allasane Kante aliyetua akitokea CA Bizertin ya Tunisia.
Fadlu ambaye msimu uliopita aliiongoza Simba kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi nyuma ya Yanga na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ameanza kuona ishara njema kutoka kwa nyota wapya katika kipindi kifupi cha mazoezi.
“Nilitarajia wangetumia muda mrefu kuzoea mfumo wetu, lakini nimefurahishwa kuona ndani ya siku chache wanajua nini wanapaswa kufanya,” alisema Fadlu huku akiongeza kuwa mawasiliano ndani ya uwanja yamekuwa bora zaidi ya alivyodhani.
Mbali na Kante na Sowah, kocha huyo aliwataja Morice Abraham ambaye alianza mazoezi na kikosi hicho tangu mwishoni mwa msimu uliopita na beki wa kimataifa wa Afrika Kusini, Rushine De Reuck.
Hata hivyo, Fadlu alikiri kuwa hali ni tofauti kwa mshambuliaji Mohamed Bajaber ambaye bado yuko kwenye hatua ya kujenga utimamu wa mwili baada ya kutoka kwenye majeraha. Bajaber ametua Simba akitokea kwa mabingwa wa Ligi Kuu Kenya, Police.
“Bajaber ana ari kubwa, lakini bado anatakiwa kuwa na subira. Tunamjenga hatua kwa hatua,” aliongeza.
Kante, kiungo mkabaji kutoka CA Bizertin ya Tunisia amekuwa kivutio katika mazoezi kutokana na uwezo wake wa kukaba kwa nguvu na kupiga pasi za haraka mbele.
“Kante ni mpambanaji wa kweli. Naamini kuna kitu tofauti atakionyesha,” alisema Fadlu.
Kwa upande wa Sowah, mshambuliaji wa Ghana, Fadlu alisema anavutiwa na namna anavyosogea bila mpira na uwezo wake wa kumalizia nyavuni.
“Sowah ana harufu ya bao. Anakimbia maeneo ambayo mabeki wengi hawawezi kuyatarajia,” alisisitiza kocha huyo.
Mazoezi ya Simba yamekuwa yakifanyika mchanganyiko yakiwamo yale ya viungo, mpira wa kasi na mbinu, huku jua la Jiji la Ismailia likiwafanya wachezaji wa timu hiyo wajihisi kama wapo Dar es Salaam.
Fadlu alisema mojawapo wa sababu za kuchagua kambi ya Misri ni kuhakikisha wachezaji wanapata muda wa kuelewana bila presha ya mashabiki na mazingira ya nyumbani.
“Hapa tuna nafasi ya kujenga familia ndani ya kikosi. Wachezaji wanakaa pamoja, wanakula pamoja na kufanya kila kitu kama timu moja,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kambi ya timu hiyo kuna uwezekano mkubwa Simba ikacheza mechi ya kwanza ya kirafiki wiki ijayo dhidi ya moja ya timu za Ligi Kuu Misri ikiwa ni fursa ya Fadlu kujaribu mastaa wapya kwenye kikosi.
Kwa sasa wachezaji wapya waliotambulishwa na Simba ni Kante, De Reuck, Morice, Hussein Daudi Semfuko, Sowah, Bajaber na Anthony Mligo.