Stars yatabiriwa kumaliza kinara kundi B

ACHANA na matokeo ya mechi za jana, Jumamosi na Taifa Stars ilikuwa na kibarua dhidi ya Madagascar, kocha wa zamani wa Yanga, Luc Eymael ameitabiria timu hiyo ya taifa la Tanzania kumaliza kinara kwenye msimamo wa kundi B.

Kocha Eymael ametoa kauli hiyo huku akisubiri mechi ya mwisho ya kundi ambayo Stars itacheza dhidi ya Afrika ya Kati Agosti 16. Hii ni baada ya Stars kufanya vizuri katika mechi zao mbili za awali na ilishinda na kuonyesha kiwango bora.

“Stars wana timu imara na kuna mabadiliko makubwa yamefanyika katika kikosi hiki. Nina uhakika kama wataendelea na namna wanavyoonyesha sasa, wana nafasi nzuri ya kumaliza kinara katika kundi hilo,” alisema Eymael.

Kocha huyo, raia wa Ubelgiji, alisema;  “Tunajua soka ni changamoto kubwa, lakini imani yangu ni Stars wataweza kupata pointi kati ya tisa hadi 12 na kuongoza kundi,” aliongeza.

Taifa Stars walionyesha umahiri mkubwa katika mechi mbili zilizopita, wakifunga mabao matatu na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu uwanjani, jambo lililowapa matumaini makubwa ya kusonga mbele katika mashindano haya ya CHAN 2024.

Mechi ya mwisho ya kundi B, itakayochezwa Agosti 16, itakuwa ni mtihani kwa Taifa Stars kuonyesha kama wanastahili nafasi ya kutinga robo fainali kwa mara ya kwanza.

“Ni muhimu kwa wachezaji kutulia, kuzingatia mafunzo ya kocha na kuwasikiliza viongozi wa timu. Hii itawawezesha kushinda mechi hii ya mwisho na kuingia robo fainali,” alisisitiza Eymael.

Hata hivyo, Stars ili imalize kinara wa kundi hilo, inatakiwa ishinde mechi zake zote kuanzia ya jana iliyopigwa katika Unjwa wa Benjamin Mkapa, huku ikiombea timu nyingine zisipate matokeo mazuri katika michezo yao.

Stars inapewa nafasi kubwa ya kufuzu robo fainali kutokana na kiwango kizuri cha nyota wake huku mashabiki wakiamini itashinda michezo yote na kuandika historia.