Dar es Salaam. Wakati Katibu wa Bunge la Tanzania, Baraka Leonard akisema Spika mstaafu wa Bunge, Job Ndugai amefariki dunia kwa shinikizo la damu kushuka lililosababishwa na maambukizi makali kwenye mfumo wa hewa, wataalamu wa afya wameuelezea ugonjwa huo.
Wakizungumza na Mwananchi leo Agosti 10, 2025 wataalamu hao wamesema shinikizo la damu la kushuka ni hali inayojitokeza wakati, shinikizo la damu likiwa chini ya kiwango kusukuma damu kufika sehemu muhimu za mwili.
Wamesema hali hiyo husababisha ogani muhimu za mwili ikiwamo ubongo, moyo na figo kukosa oksijeni ya kutosha, hivyo huweza kusababisha kifo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Elisha Osati amesema mtu anapopata maambukizi makali kwenye mfumo wa hewa humletea ‘septic shock’ hali inayosababisha presha yake kupungua.
Amesema ‘septic shock’ husababisha maambukizi kwenye mwili ambayo husababisha kutolewa kwa vichocheo vingi, vinavyosababisha mishipa ya damu kutanuka.
“Ikitanuka inasababisha presha ya damu kuwa chini sana, presha inapungua sababu mishipa imepungua wakati mwili unapambana na bakteria kwa ajili ya kuwaondoa inazalisha aina mbalimbali za homoni, vichocheo na hizo zinatoka kwa wingi na kusababisha mishipa kutanuka na inaweza kutoboka pia.
“Ukipata hiyo maana yake presha yake inapungua, yaani unaweza kupata maambukizi makali ambayo yanasababisha ‘inflammation’ si uvimbe lakini mishipa ya damu inaweza ikatanuka ghafla,” amesema.
Dk Osati amesema kutanuka ghafla kwa mishipa, maana yake inaweza kusababisha presha kupungua na ikitokea mishipa inashtuka na kutanuka, ikitanuka inasababisha presha kupungua.
Amesema ikipungua maana yake damu haiendi kirahisi kwenye viungo mbalimbali muhimu kama kwenye mishipa ya moyo, mishipa ya ubongo na mishipa ya figo, hivyo kama haiendi vizuri maana yake oksijeni pia haiendi vizuri.
“Ukipata tatizo hilo ogani zinakosa hewa, inaweza kusababisha kifo haraka sana, sawasawa na maambukizi ya njia ya hewa kama nimonia kali sana ambayo ikaleta reaction kwenye mwili mzima na kusababisha damu kutokwenda katika ogani muhimu kama ubongo, moyo na figo, zikikosa damu ya kutosha mtu anaweza kufariki ghafla inawezekana kuwa chanzo cha kifo,” amesema Dk Osati.
Amefafanua kuwa, hali hiyo inaweza kusababisha kufeli kwa njia ya hewa, kwa kutopokea oksijeni ya kutosha na kabonidayoksidi ya kutosha ikibaki kwenye mwili.
Dk Osati amebainisha kuwa, mara nyingi changamoto hiyo huweza kuwapata watoto na wazee, kwa sababu wazee miili yao inakuwa imeanza kuzeeka na watoto kinga zao bado hazijawa imara.
Daktari mshauri mwandamizi wa magonjwa ya ndani na moyo, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ambaye pia ni mhadhiri wa vyuo vikuu mbalimbali vya tiba, Profesa Harun Nyagori amesema shinikizo la damu la kushuka ni eneo pana sana.
Amesema shinikizo la damu la kushuka linapotokea linategemeana na umri wa mtu na zipo sababu nyingi kwa shinikizo la damu la juu na shinikizo la damu la kushuka.
“Shinikizo la kushuka lina sababu za kibaolojia, huwezi kuzungumza moja kwa moja. Mpaka presha ishuke kuna vitu hufanyika na kuna sababu zaidi ya 50 na hiyo ni fiziolojia ni kama ukiuliza kwanini mtu anapata usingizi ni mchakato mrefu sana ili mtu alale,” amesema Profesa Nyagori.
Akizungumza leo aliposoma wasifu wa marehemu Ndugai katika viwanja vya Bunge ilipofanyika shughuli ya kitaifa ya kumuaga kabla ya kwenda kuzikwa kijijini kwao Kongwa jijini Dodoma, Leonard amesema,“kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, alifariki kutokana na shinikizo la damu kushuka sana, iliyosababishwa na maambukizi makali kwenye mfumo wa hewa.”