Zitto ajiapiza kwa Mpina | Mwananchi

Pemba. Kiongozi mstaafu wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amesema viongozi wa chama hicho, walifanya tathimini ya kina hadi kumpa kijiti Luhaga Mpina cha kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, akiwataka wanachama wao kutokuwa na wasiwasi na mtiania huyo.

Kutokana hofu na shaka walionayo, Zitto amewaambia Wazanzibari kuwa viongozi wa chama hicho wanabeba dhamana kuhusu ujio wa Mpina ambaye amepitishwa kuwania urais wa Tanzania.

Zitto ameeleza hayo leo Jumapili Agosti 10, 2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Tibirinzi Pemba wakati wakihitimisha mchakato wa kuwatambulisha watiania wa urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mpina na Zanzibar, Othman Masoud.

Utambulisho wa watiania hao ulianzia jana Jumamosi mjini Unguja Agosti 9, 2025 na walipokewa na umati wa wananchi. Kama ilivyokuwa Unguja, Pemba nako umati wa watu waliojitokeza pembezoni mwa barabara kuanzia uwanja wa ndege hadi Tibirinzi.

Katika maelezo yake, Zitto amesema anaelewa wasiwasi wa wananchi wa Zanzibar, uliotokana na historia ya huko nyuma ya watu waliohamia chama hicho, lakini mambo yalikuwa tofauti na matarajio ya chama hicho.

Ingawa mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Mjini hakufafanua, historia inaonesha wapo makada waliotoka CCM na kuwania nafasi za juu za chama na walikuja na ahadi lukuki lakini hawakuweza kuzitekeleza.

Zitto amesema anamjua vyema Mpina tangu walivyokutana naye kwa mara kwanza mwaka 2005 bungeni na kufanya kazi kwa pamoja za kibunge hadi mwaka 2020.

“Mpina akikwambia nyeupe ni nyeupe, akikwambia nyeusi ni nyeusi. Naelewa na viongozi wenu wanaelewa, wasiwasi wenu wa huko tulikotoka. Lakini tumefanya tathimini ya kutosha, tunamchukulia dhamana Mpina kwa sababu tunamwamini,” amesema.

“Historia yake ni mwanasiasa mwenye msimamo, anayechukizwa na ufisadi na ubadhirifu katika Taifa letu. Ni historia ya mwanasiasa anayetaka kuona mabadiliko katika Taifa, aliyeamua kuungana na wenzake ili kutekeleza wajibu muhimu sana,” amesema Zitto.

Amewataka Wazanzibari kumpokea Mpina kwa sababu ni mwanasiasa ambaye amewaungana na wenzake ili kuleta mabadiliko katika Taifa hili, hivyo vijana wenzake wa chama hicho na Watanzania wampokee.

Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesema siku 60 za kampeni za uchaguzi mkuu kuanzia Agosti 28 watazitumia kueleza walipokosea chama tawala na namna ya chama hicho kitakavyofanya baada ya kushika madaraka Oktoba mwaja huu.

“Tunataka kutimiza ndoto za Maalim Seif (Sharif Hamad- mwenyekiti wa zamani wa ACT- Wazalendo) za kuifanya ndoto ya kuifanya Unguja na Pemba kuwa Singapore ya Afrika,” amesema Jussa.