Beki Mghana kumchomoa mtu Yanga, ishu nzima ipo hivi!

KUNA pishi linapikwa pale Jangwani asikuambie mtu! Unakumbuka ile stori ya beki Mkongomani anayekipiga Sauzi ambaye Yanga inamfukuzia kuja kutimba pale kati na kina Dickson Job pamoja na Ibrahim Hamad ‘Bacca’?

Basi, chama hilo unaambiwa liko katika mipango mingine kabambe ya kusika lile aeneo la ulinzi ambalo msimu uliopita kuna mechi moja lililitia aibu baada ya kuruhusu mabao 3-1 kutoka kwa Tabora United kutoka na mabeki wake visiki kuwa majeruhi.

Lakini, licha ya kuwepo kwa taarifa kwamba Yanga imepanga kumfuata beki Afrika Kusini, lakini Mwanaspoti imepenyezewa kwamba Singida Black Stars ina mpango wa kumtoa kwa mkopo beki wa kati Mghana, Kwabena Frank Assinki ili ajiunge na mabingwa hao wa soka nchini.

Hata hivyo, ujio wa Mghana huyo huenda ikala kichwa cha beki wa kulia aliye majeruhi, Yao Kouassi kutokana na takwa la kikanuni kwa wachezaji wa kigeni ambao unahitaji kila timu wasizidi 12.

Wikiendi iliyopita Mwanaspoti ilipenyezewa kwamba Yanga imeamua kumpandia ndege beki Nathan Idumba Fasika anayeichezea Cape Town City ya Afrika Kusini ili kumsajili kabla ya dirisha halijafungwa mwezi ujao kwa lengo la kuimarisha eneo la ulinzi.

Hata hivyo, kabla ya jambo hilo halijatekelezwa, tayari Yanga imepata mteremko baada ya Singida kudaiwa ipo tayari kumuachia Assinki kwa mkopo ili ajiunge na mabingwa hao mara nne mfululizo wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).

Assinki aliyezaliwa Aprili 15, 2002, huku Ghana alijiunga na SBS katika dirisha dogo la msimu uliopita Desemba 24, 2024 kutoka Inter Allies ya Ghana na tangu ajiunge na timu hiyo ameonyesha kiwango kizuri kilichowavutia Yanga ili atue kuchuana na kina Dickson Job, Ibrahim Bacca na Bakari Mwamnyeto.

“Beki huyo ataingia nchini muda wowote akitokea kwao Ghana, anakwenda kujiunga na Yanga ambayo imehitaji huduma yake kwa mkopo, kwa sasa kinachoendelea ni kukamilisha taratibu zinazotakiwa,” kimesema chanzo kutoka ndani ya Yanga.Chanzo hicho kimesema mpango huo ukienda sawa ataondolewa katika mfumo wa usajili beki wa kati Yao Kouassi aliyejiunga na Yanga Julai 14, 2023.

“Sababu ya kutaka kumuondoa Yao ni kutokana na changamoto ya majeraha ya hapa na pale, hivyo anahitajika mchezaji aliyefiti kwa ajili ya kukabiliana na ugumu wa mashindano,” kimesema chanzo hicho na kuongeza:

“Yao ni beki mzuri ana kasi, anatumia nguvu hivyo kumuondoa katika mfumo hakumanishi ameshuka kiwango, isipokuwa Yanga ina mpango wa kupigania mataji ya ndani na nje, lazima kila nafasi iwe na wachezaji imara.”

Msimu wa 2023-2024 ambao Yao alikuwa bora zaidi alifunga bao moja, alifanya faulo 18, hakuwa na kadi, aliingilia mpira mara 24, alizuia mashambulizi mawili, aliokoa hatari tatu, alishinda mipira ya hewani sita, ile ya chini mitatu na kucheza mechi 25.