CAF yasitisha uuzaji tiketi za CHAN Kenya

KWA mujibu wa taarifa kutoka Kenya, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limesitisha uuzaji wa tiketi kwa mechi zote zijazo zitakazochezwa kwenye Uwanja wa Moi International Sports Centre, Kasarani, ikiwamo ya Jumapili ijayo ya Harambee Stars dhidi ya Zambia.

Sababu ya CAF kusitisha uuzaji wa tiketi ni kutokana na dosari kubwa za usalama zilizotokea kwenye mchezo wa Harambee Stars dhidi ya Morocco jana.

Tukio hilo lililotokea Jumapili lilihusisha mamia ya mashabiki wa Kenya kunyimwa kuingia uwanjani licha ya kuwa na tiketi zilizodhaniwa ni halali.

Hali hiyo ilisababisha vurugu na uvunjaji wa lango na kuingia kwa mashabiki wasio na tiketi, kuzidi kwa idadi ya watu kuliko uwezo wa uwanja, mashabiki kuvamia chumba cha wanahabari na polisi kutumia mabomu ya machozi kutuliza vurugu.

Kamati za nidhamu na usalama za CAF zinachunguza tukio hilo na zitaamua hatua zinazofuata.

Katika baruapepe, kampuni ya Mookh Africa inayohusika na huduma za tiketi imethibitisha uuzaji wa tiketi umesitishwa hadi waandaaji watakapotoa taarifa mpya.

“Baada ya dosari za usalama Kasarani jana, uuzaji wa tiketi kwa michezo ya Kasarani umesitishwa hadi taarifa mpya kutoka kwa waandaaji,” Mookh Support Team imesema.

Tukio hili limezua hofu kwa CAF, ambayo tayari imeitoza Shirikisho la Soka Kenya (FKF) faini ya Sh2.5 milioni kwa udhibiti hafifu wa watu. CAF imeonya kutoa adhabu kali zaidi iwapo vurugu kama hizo zitajirudiwa katika mashindano haya.