CP. WAKULYAMBA ALITAKA JESHI LA UHIFADHI KUJIANDAA KUTEKELEZA DIRA YA 2050

………….

Sixmund Begashe, Arusha

Taasisi zinazounda Jeshi la Uhifadhi zimetakiwa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025/2050 (Dira ya 2050) ili kuwa tayari kwa utekelezaje wake kwenye masuala yote yanayo husu Wizara ya Maliasili na Utalii hususani katika maeneo ya uhifadhi wa urithi wa Maliasili za wanyamapori, Misitu na Malikale.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili kwenye kikao kazi kati ya Wizara na Jeshi la Uhifadhi Mkoani Arusha ambacho kiliitishwa kwa lengo la kupata uwelewa wa pamoja wa uimarishaji wa uhifadhi endelevu wa maliasili kwa kuzingatia maelekezo ya Tume ya Haki Jinai.

CP. Wakulyamba amesema kuwa, utekelezaji wa Dira ya 2050 kwa Jeshi la Uhifadhi itakuwa ni njia sahii ya kuunga mkono jitihada kubwa zonazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha nchi na wananchi wanapata maendeleo kupitia urithi wa Maliasili za nchi.

Aidha, CP. Wakulyamba amesisitiza kuwa, japo kuwa Jeshi hilo linafanya kazi nzuri, ni lazima Taasisi zake zote zishikamane kwenye ulinzi wa Maliasili dhidi ya watu wachache wenye nia ovu dhidi ya Maliasili nchini.

Amezielekeza taasisi hizo pia kutumia tafiti za ndani katika kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta ya Uhifadhi wa Maliasili kwa kuwa Wizara hiyo inawataalam wabobezi kwenye nyanja za Uhifadhi, Utalii na Malikale.

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa taasisi za Jeshi la Uhifadhi, Kamishna Mkuu wa Uhifadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dossantos Silayo ameuhakikishia uongozi wa Wizara kuwa watasimamia vyema maelekezo yaliyotolewa hasa ya Utekelezaji wa Dira ya 2050, utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai pamoja na kusimamia nidhamu na uadikifu kwa askari wa Jeshi hilo.