Elimu ya amali inaweza kututoa Watanzania

Dar es Salaam. Katika dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi kubwa, siyo tu maarifa ya kinadharia yanayohitajika, bali pia uwezo wa kivitendo, yaani ujuzi wa amali. 

Elimu ya amali, ambayo mara nyingi hufananishwa na elimu ya ufundi au elimu ya ujuzi, ndio njia bora ya kuandaa vijana kwa maisha ya kazi, uvumbuzi, na kujitegemea.

 Elimu hii inawapa wanafunzi stadi zinazowezesha kutumia mikono yao, akili zao kwa vitendo, na ubunifu wao kutatua matatizo halisi ya jamii. Kwa mantiki hii, elimu ya amali inaweza kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa letu.

Kwa muda mrefu, mfumo wa elimu nchini umeweka mkazo mkubwa katika elimu ya nadharia, huku ukipuuza au kutoipa uzito stahiki elimu ya ujuzi.

 Hali hii imechangia kuzalisha wahitimu wengi wasio na uwezo wa kujiajiri au kuchangia moja kwa moja katika shughuli za uzalishaji mali.

 Kila mwaka, maelfu ya vijana wanaomaliza elimu ya sekondari na vyuo vikuu huingia sokoni wakiwa na vyeti mikononi, lakini hawana ujuzi unaohitajika na soko la ajira. Hii imesababisha kuongezeka kwa ukosefu wa ajira na kutegemea Serikali au sekta binafsi kwa ajira chache zilizopo.

Tofauti na hali hiyo, elimu ya amali inalenga kumjenga mwanafunzi kuwa mtendaji. Inajikita katika stadi za maisha, teknolojia, ufundi, kilimo, biashara ndogondogo, uhandisi wa kawaida, na kazi nyingine za mikono ambazo ni msingi wa maendeleo ya jamii yoyote. 

Kwa mfano, kijana aliyepitia mafunzo ya useremala, fundi wa magari, ushonaji, uashi, umeme wa majumbani au teknolojia ya habari, ana nafasi kubwa ya kujiajiri na hata kuwaajiri wengine. Elimu hii humwezesha kijana kuwa mbunifu na mjasiriamali, badala ya kuwa mtegemezi wa ajira.

Dunia ya sasa, hasa katika karne ya 21, inathamini zaidi ujuzi kuliko kiwango cha maarifa ya kinadharia tu. Kampuni kubwa na taasisi mbalimbali za kimataifa zimeanza kupima uwezo wa mtu kwa kuzingatia anachoweza kufanya kwa vitendo, si kwa kutazama tu vyeti alivyovipata darasani.

 Hii ni kwa sababu maarifa peke yake hayatoshi; kinachohitajika ni mtu anayeweza kutumia maarifa hayo kwa ufanisi kutatua changamoto za kweli. 

Ndio maana nchi zilizoendelea zimewekeza sana katika elimu ya amali na mafunzo ya ufundi, kama njia ya kuhakikisha rasilimali watu yao inakuwa na uwezo wa kuzalisha mali na kuchochea uchumi.

Kwa Tanzania, elimu ya amali inaweza kuwa mkombozi wa kiuchumi. Kwa kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kupitia ujuzi wa kazi mbalimbali, tutapunguza tatizo la ukosefu wa ajira, kuongeza pato la mtu binafsi na taifa kwa ujumla, na kuimarisha maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati. Vijana wanaojifunza ufundi wanakuwa sehemu ya mnyororo wa uzalishaji ambao unatoa huduma na bidhaa zinazotegemewa na jamii. 

Kwa mfano, mafundi umeme, mafundi bomba, wakulima wa kisasa, wabunifu wa mitindo, na wapishi wa kitaalamu wote wana mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.

Maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kukuza ujuzi kwa Watanzania yanapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote. 

Kupitia ajenda yake ya ujenzi wa uchumi shindani, Serikali imeanza kuwekeza katika vyuo vya ufundi na kuanzisha programu mbalimbali za mafunzo ya amali. 

Hii ni hatua muhimu sana kwani inadhihirisha dhamira ya dhati ya kuimarisha nguvu kazi ya Taifa. Ikiwa tutaliendeleza hili kwa uwekezaji endelevu katika vifaa, walimu wenye ujuzi, miundombinu bora na mitalaa inayokidhi mahitaji ya soko, Tanzania inaweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Zaidi ya hapo, elimu ya amali ina nafasi ya kubadili mitazamo ya kijamii kuhusu mafanikio. Kwa muda mrefu, mafanikio yamekuwa yakihusishwa na kazi za ofisini au cheo kikubwa serikalini. 

Lakini ukweli ni kwamba mafanikio yanaweza kupatikana kupitia kazi yoyote halali inayofanywa kwa bidii, uadilifu na ubunifu. Fundi seremala anaweza kujenga biashara kubwa, mjasiriamali mdogo anaweza kuwa muuzaji mkubwa wa bidhaa sokoni, na mpishi anaweza kuwa mmiliki wa mgahawa maarufu.

 Elimu ya amali inafungua njia hizi zote kwa kuwajengea vijana ujuzi wa kufanya kazi kwa kujitegemea na kwa ubora unaohitajika duniani.

Katika mazingira ambayo teknolojia inabadilika kwa kasi, elimu ya amali pia ina nafasi muhimu ya kuwawezesha vijana kuendana na wakati. 

Mafunzo ya teknolojia ya habari, uundaji wa programu, uchapaji kwa kutumia teknolojia ya  3D, robotiki na ufundi wa kisasa wa magari ni maeneo ambayo yanahitaji ujuzi maalum na yanatoa fursa nyingi za ajira.

 Haya yote ni maeneo yanayoweza kufundishwa kupitia mifumo ya elimu ya amali, ambayo inajali mazoezi ya vitendo zaidi kuliko nadharia pekee.

Nisisitize elimu ya amali au ufundi si chaguo la pili au la wanyonge kama ilivyoaminika kwa muda mrefu. Ni njia halali, ya heshima na yenye tija ya kufanikisha maisha bora kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla. 

Tanzania ikiwa na vijana wengi waliobobea katika elimu ya amali, itakuwa na msingi imara wa maendeleo endelevu. 

Hii ndiyo dira ya karne ya 21,  karne ya ujuzi, si maarifa ya darasani pekee. Kwa hiyo, ni wajibu wetu kama Taifa kuwekeza, kuhamasisha, na kuiheshimu elimu ya amali kama nguzo ya mafanikio yetu ya baadaye.