SAA chache tangu kufanyika kwa droo ya mechi za raundi za awali za michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu ikiwamo Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu wa 2025-2026, kocha mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi amekiri kuna ugumu kuwakabili Rayon Sports.
Singida itavaana na Rayon ya Rwanda katika mechi ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika na Gamondi amefunguka ugumu ulio mbele yao, huku akijivunia ubora na uzoefu wa nyota wake.
Singida BS itavaana na Wanyarwanda hao Septemba 19-21 na zitarudiana Septemba 26-28 ili mshindi kutinga raundi ya pili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema ni mechi ngumu kwa Singida, lakini wanatakiwa kucheza mchezo wa upinzani ili kujiweka kwenye ushindani na kuikuta timu hiyo.
“Singida Black Stars ni wawakilishi wa Tanzania ili kuwa bora wanatakiwa kucheza na timu ngumu hivyo hiki ni kipimo sahihi kwetu tunahitaji kufanya maandalizi makubwa kabla ya kuwakabili,” alisema Gamondi na kuongeza;
“Tuna wachezaji wazuri na wazoefu naamini mipango sahihi ndiyo itakayotupa matokeo mazuri tunatakiwa kuwaheshimu wapinzani kabla ya kuangalia dakika 90 pekee.”
Gamondi alisema mashindano hayo hayana mpinzani rahisi wanaenda wakijua wanaenda kushindana na kuiwakilisha Tanzania maandalizi yanayoendelea sasa yatatoa picha wataenda kufanya jambo gani kubwa.
“Nafahamu hayo mashindano ni makubwa na yana timu bora ambazo pia zina malengo kama yetu hivyo naamini kujiandaa vizuri kutatoa picha ya nini tunaenda kukifanya huko,” alisema Gamondi ambaye mara mbili wakati akiwa Yanga akiiwezesha kuvuka raundi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika na kutinga makundi ikiwamo misimu miwili ilipofika hadi robo fainali.