Kanoute asaini miwili Azam FC

ALIYEWAHI kuwa kiungo wa Simba, Sadio Kanoute muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa kuitumikia Azam FC baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.

Kiungo huyo anajiunga na matajiri wa Dar es Salaam akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na JS Kabylie ya Algeria ambayo aliitumikia msimu uliopita.

Kanoute tayari yupo nchini na ameshafanyiwa vipimo vya afya na kusaini mkataba wa miaka miwili, na muda wowote atatangazwa na ataungana na timu ambayo imeweka kambi mkoani Arusha.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo kimeihakikishia Mwanaspoti kuwa mchezaji huyo atahudumu Azam FC hadi 2027.

Kanoute alicheza Ligi Kuu Bara akiwa Simba baada ya kuhudumu kwa misimu mitatu tangu 2021 akitokea Al Ahly Benghazi ya Libya.

Kiungo huyo raia wa Mali baada ya kutua ardhi ya Tanzania, alisema anafurahia kurejea nchini kujiunga na Azam FC.

“Nina furaha kuwa hapa Tanzania ndani ya Azam FC. Najisikia nipo nyumbani na nitajitahidi kujitoa kadri niwezavyo kuipandisha timu na kuwafanya mashabiki kuwa na furaha,” amesema.

Ujio wa kiungo huyo ndani ya kikosi cha Azam FC unaongeza idadi ya namba kwenye eneo la kiungo ambalo tayari lina James Akaminko, Sospeter Bajana, Adolph Mtasingwa, Yahya Zayd na Ever Meza.