MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Kelvin John, anazidi kung’ara baada ya juzi kufunga mabao mawili na kuipatia ushindi timu yake AaB Fodbold ya Denmark.
Msimu uliopita, timu hiyo ilimaliza mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Denmark na kushushwa daraja, hivyo sasa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Ligi hiyo inaendelea ikiwa tayari zimechezwa mechi nne, na mabao aliyofunga juzi John yameipa ushindi wa kwanza timu hiyo, ambayo kwa sasa ipo nafasi ya nane kati ya timu 12 kwenye msimamo wa ligi.
Baada ya mechi kwisha timu ilimposti kwenye mitandao ya kijamii na kuandika: “Mchezaji bora wa mechi, mfungaji wetu wa mabao mawili, Kelvin John, amejinyakulia taji la mchezaji bora wa AaB wa mechi hii baada ya kura zako kupitia APP.”
Pia Kelvin ndiye alikuwa ‘Man of the Match’ na utaratibu wa kumpata mchezaji bora wa mechi nchini Denmark ni kwa mashabiki kupiga kura kupitia APP, na anayepata kura nyingi hutangazwa mshindi.
Kwa sasa, mchezaji huyi anakubalika na mashabiki wa timu hiyo, jambo linalothibitishwa na namna wanavyomshangilia majukwaani anapofunga.
Nyota huyo wa Taifa Stars amekuwa na mwendelezo mzuri tangu msimu ulipoanza, ambapo kwenye mechi nne amefunga mabao matatu na kutoa asisti moja.
Mwezi Julai pia aliibuka na tuzo ya mchezaji bora wa mwezi baada ya kufunga bao moja na kutoa asisti moja, jambo linaloonyesha mwanzo mzuri wa msimu huu.