Mwanza. Kichwa cha dereva bodaboda, Dickson Yusuph (24), mkazi wa Mtaa wa Shadi, Kata ya Luchelele, jijini Mwanza, kimepatikana baada ya watuhumiwa wawili kuliongoza Jeshi la Polisi hadi msitu wa Nsumba walipokificha, baada ya kukitenganisha na kiwiliwili.
Dickson alipatikana akiwa ameuawa Agosti 9, 2025, katika Mtaa wa Malimbe, Kata ya Luchelele, Wilaya ya Nyamagana, kando ya barabara ya Luchelele, mwili wake ukiwa hauna kichwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 11, 2025, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Gideon Msuya, amesema baada ya uchunguzi wa kina, marehemu alitambulika na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wawili ambao ni Oscar Emmanuel (20) na Edwin Petrol (22), wote wakazi wa Shadi.
Msuya amedai wakati wa msako, polisi walipata mali za marehemu, ikiwamo pikipiki aina ya TVS yenye namba za usajili MC 715 ENN na simu aina ya Infinix Hot 10, huku uchunguzi wa awali ukionesha chanzo cha mauaji ni wivu wa mapenzi kati ya marehemu na mke wa mmoja wa watuhumiwa wa mauaji hayo.
“Uchunguzi wa awali ulionesha tukio lilihusiana na wivu wa mapenzi, na kwa msaada wa taarifa kutoka kwa wananchi tulibaini jina la marehemu na kuanza msako mkali wa wahusika,” amesema Msuya.
Watuhumiwa walivyokamatwa, kuuawa
Amesema Agosti 10, 2025 mchana, polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili, wote wakulima na wakazi wa Shadi.
Baada ya mahojiano ya kina, walikiri kuhusika na mauaji ya Dickson na kueleza kuwa walimvamia, kumkata kwa panga na kisha kuondoka na kichwa pamoja na mali zake.
Amedai walikiri kuficha kichwa chake kwenye msitu wa Nsumba, kisha kukubali kuonesha walipokificha kichwa na mali hizo, jambo lililowalazimu polisi kuwasindikiza hadi eneo hilo.
Hata hivyo, usiku huo, wakati polisi wakioneshwa na watuhumiwa sehemu walipoficha kichwa cha Dickson, kundi la wananchi liliwafuata na kuanza kuwashambulia watuhumiwa hao.
“Wakati watuhumiwa wanaonesha mali za marehemu Dickson ndani ya msitu huo wa Nsumba, lilijitokeza kundi la wananchi waliopata taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kuanza kuwashambulia askari Polisi pamoja na watuhumiwa hao.
“Askari walijitahidi kuzuia wananchi wasiwashambulie watuhumiwa huku wakiepusha kutokea kwa madhara makubwa, endapo wangetumia nguvu kubwa ya silaha za moto walizokuwa nazo, wangeweza kuleta madhara makubwa kwa watu wengi waliokuwa wamekusanyika na kufuatilia tukio hilo,” amesema Msuya.
Amesema katika purukushani hizo watuhumiwa wote wawili waliuawa na wananchi wenye hasira, huku askari wawili wakijeruhiwa na walipelekwa hospitali kwa matibabu.
“Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo hospitali ya kanda Bugando kwa ajili ya kutambuliwa na kufanyiwa uchunguzi… kichwa cha marehemu Dickson pia kimehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi,” ameongeza.
Amesema mali za marehemu, zikiwemo pikipiki na simu ya mkononi, zimepatikana na taratibu za kisheria zikiendelea.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Mtaa wa Silivini, Ramadhan Malugu, amesema walisikia milio ya sauti inayodhaniwa kuwa ya risasi, hali iliyozua taharuki kwa wakazi wa mtaa huo.
“Hao watu walikamatwa wakiwa na kichwa walichokificha. Hasira za wananchi zilipanda kwa sababu marehemu alikuwa kijana anayefahamika na kupendwa na wenzake wa bodaboda. Wengine walihisi bora wauawe papo hapo kuliko kupelekwa mahakamani,” amedai Malugu.
Mkazi wa Luchelele, Suwed Kanyima, amesema milio ya risasi na vishindo vilianza kusikika kati ya saa nne na saa tano usiku.
“Niliposikia nilikuwa na hofu nikiamini ni majambazi, lakini ilipofika asubuhi baadhi ya watu waliowaona walisema ni Jeshi la Polisi.
“Tunapenda waendelee kufanya uchunguzi ingawaje hatujui wanafanyeje hata kufika na kuchukua hatua ni ishara ya kwamba jeshi lipo kazini.
“Sisi jamii hatuna chombo kingine cha kuamini kwa sababu jeshi ndio linawajibika na usalama wetu, hata kama jamii imepungukiwa na amani, iwe na imani na Jeshi la Polisi lifanye kazi yake,” amesema.
Mkazi wa mtaa wa Kisoko, Dickson Ndaki, aliyewahi kuwa balozi, amesema matukio ya namna hiyo yamekuwa yakijitokeza kutokana na mwingiliano wa watu, na hutumia pori hilo kufanya uhalifu.
“Kipindi cha nyuma matukio kama haya hayakuwepo, kwa mfano hawa wasomi wana vitu vya gharama, kwa hiyo wahalifu wakiona eneo hili ni tulivu wanakuja kufanya mambo yao huku,” amesema.
“Matukio kama haya hata mwaka jana lilikuwepo tukio la mtu mmoja alionekana ametupwa kwenye josho la ng’ombe, pia matukio mengine ambayo hujitokeza na watu huwa hawayatolei taarifa,” amesema.
Amesema kadri matukio hayo yanapozidi kujitokeza, watu wanaishi kwa hofu hata kuanza kufanya shughuli zao mapema alfajiri kwa kuogopa, akieleza kuwa baadhi ya matukio hayatolewi taarifa kutokana na watu kuogopa kuingia kwenye tuhuma.
“Kuna matukio mengine watu wengine huwa hawataki kuzungumza kwa sababu ukishasema hivyo lazima ushirikiane na askari kwa ajili ya kutoa ushahidi,” ameeleza.
Ameshauri Serikali iangalie utaratibu wa msitu huo ujengwe ili kuwaogopesha wahalifu wanaopenda kutumia eneo hilo kufanya matukio ya kikatili.
Kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za matukio ya uhalifu na ajali za barabarani za mwaka 2024 iliyotolewa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), jumla ya watu 103 waliripotiwa kuuawa mkoani Mwanza kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo wizi, ukabaji, mapenzi na imani potofu.
Katika taarifa hiyo, kati ya waliouawa wanaume walikuwa 70, huku wanawake wakiwa 33.