Kipa Pamba awapiga mkwara Diarra, Moussa Camara

KIPA wa Pamba Jiji, Yona Amos aliyemaliza nafasi ya nne kwa makipa waliokuwa na ‘clean sheets’ nyingi baada ya Moussa Camara wa Simba, Diarra Djigui na Patrick Munthari amesema msimu wa 2025-26 ataendelea alipoishia mipango ni kuongeza namba.

Kipa huyo aliyeshika namba mbili ya makipa wazawa waliofanya vizuri msimu uliopita akiwa na clean sheet 11, nyuma ya Munthari wa Mashujaa, aliyekuwa na 14, aliliambia Mwanaspoti, malengo ya msimu ulioisha hayajatimia anajiandaa kuhakikisha msimu ujao anaongeza namba zaidi.

“Msimu uliopita ulikuwa na ushindani mkubwa niliweza kufikia namba hizo, malengo yangu sasa ni kupambana nisogee hatua nyingine msimu ujao, hilo linawezekana nikiweka juhudi zangu huko,” alisema Yona na kuongeza;

“Msimu uliopita umetoa picha ya ni namna gani tunatakiwa kujipanga kwani tunatarajia ushindani mkubwa mipango na mikakati yangu ni kuwa bora na kufikia malengo ya kuwa kipa bora wa msimu.”

Yona alisema bado yupo ndani ya kikosi cha Pamba Jiji na anaendelea na maandalizi ya msimu mpya akiwa na malengo ya kuendelea kuipambania timu hiyo iweze kufanya vizuri msimu ujao.

“Nipo kambini naendelea na mazoezi ni wazi kuwa bado ni mchezaji wa Pamba Jiji chini ya kocha mpya Francis Baraza tukutane msimu ujao,” alisema kipa huyo.