Kundi la askari Mali lakamatwa kwa kutaka kupindua Serikali

Dar es Salaam. Serikali ya kijeshi ya Mali imelikamata kundi la wanajeshi wanaoshukiwa kuwa na njama ya kuipindua serikali hiyo inayoongozwa na Rais Assimi Goita.

Kwa mujibu wa DW, miongoni mwa waliokamatwa ni Jenerali Abass Dembele, Gavana wa zamani wa Jimbo la Mopti akiwa pia ni ofisa wa kijeshi anayeheshimika.

Hayo yameelezwa jana Jumapili, Agosti 10, 2025 na shirika la habari la AFP likinukuu vyanzo kadhaa vilivyosema kuwa karibu askari 50 wametiwa nguvuni.

 “Kwa karibu siku tatu zilizopita, kumekuwa na kukamatwa kwa watu wanaohusishwa na jaribio la kuvuruga nchi. Kumekuwa na takriban makumi ya watu waliokamatwa,” chanzo cha usalama cha Mali kiliiambia AFP.

Hata hivyo, tangu kushika madaraka kuiongoza Mali kupitia mapinduzi ya mfululizo mwaka 2020 na 2021, utawala wa kijeshi wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi umedaiwa kuzidisha ukandamizaji wa wakosoaji wake licha ya machafuko yaliyoenea ya wanajihadi.

Imeelezwa tangu mwaka wa 2012, Mali imekumbwa na migogoro katika nyanja mbalimbali, huku wanamgambo wanaohusishwa na Al-Qaeda au makundi ya Islamic State wakitekeleza mashambulizi makali katika taifa hilo.

Aidha baada ya mapinduzi, serikali hiyo ya kijeshi iliipa kisogo Ufaransa, ikisema nchi hiyo inapaswa kuwa huru kutoka kwa mtawala wake huyo wa zamani wa kikoloni, kama walivyofanya washirika wenzake wanaoendeshwa na jeshi huko Niger na Burkina Faso.

Baadaye ilidaiwa kuanzisha uhusiano na washirika wapya hasa Russia ambayo mamluki kutoka kundi la wanamgambo la Wagner na mrithi wake Africa Corps wamesaidia jeshi kupambana na wanajihadi na maadui wengine wa ndani.