……………………….
Makamu
wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ni
muhimu Jeshi la Polisi kuimarisha ushirikiano wa karibu na wadau wote wa
uchaguzi, hatua ambayo itasaidia kuhakikisha kila mdau anatendewa haki, na
kuondoa tofauti zinazoweza kusababisha migongano.
Makamu wa Rais ametoa wito huo
wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi
unaofanyika katika ukumbi wa Chuo Cha Polisi (CCP) Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Amesema Baadhi ya maeneo muhimu ya ushirikiano ni pamoja na kuhakikisha
mikutano ya kampeni inafanyika kwenye maeneo yaliyoruhusiwa na ndani ya muda
uliopangwa, Kuzuia maandamano yasiyo na kibali, kuimarisha ulinzi wa wagombea
na viongozi wa vyama vya kisiasa, bila kujali vyama vyao au itikadi zao pamoja
na kudhibiti misongamano mikubwa ya watu ili kuhakikisha shughuli nyingine za
kijamii na kiuchumi zinaendelea bila usumbufu.
Pia Makamu wa
Rais amelitaka Jeshi la Polisi kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na taasisi nyingine za Serikali ili
kujiandaa vyema kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika
kufuatilia taarifa mbalimbali zenye mlengo wa uchochezi, zinazotolewa kupitia
mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari. Amesema kwa kutumia
teknolojia za akili bandia baadhi ya watu wanaweza kusambaza picha au video za
uongo za wagombea wa vyama vya siasa, jambo linaloweza kuleta madhara makubwa
kwa amani na utulivu wa jamii.
Makamu wa Rais amesema Jeshi la
Polisi linapaswa kujiandaa kikamilifu kufanya doria ya mtandao ili kubaini na
kuchambua machapisho, picha, na video zenye viashiria vya uvunjifu wa sheria,
na kuchukua hatua za kisheria kwa haraka.
Vilevile, Makamu wa Rais
amesisitiza Jeshi la Polisi lishirikiane kwa karibu na wadau wengine wa
uchaguzi, ikiwemo TAKUKURU na vyombo vingine vya usalama, ili kudhibiti vitendo
vya Rushwa katika kipindi cha uchaguzi. Ameongeza kwamba ni muhimu Jeshi la Polisi likijumuisha Polisi
Jamii lishirikiane kwa karibu na TAMISEMI katika kusimamia usalama, hasa katika
ngazi za Kata, Shehia, Vijiji na Mitaa.
Makamu wa Rais amelitaka Jeshi la
Polisi kusimamia vema utekelezaji wa sheria ya uchaguzi na sheria nyingine za
nchi. Amesema ni wajibu wa Jeshi la Polisi na wadau wengine wa uchaguzi, kuielewa
vizuri Sheria ya Uchaguzi na kusimamia utekelezaji wake, ili kuepuka kuonea
watu na kuvuruga uchaguzi.
Aidha ametoa wito kwa wananchi na viongozi wa vyama
vya siasa kuepuka kujichukulia sheria mkononi pale wanapoona ukiukwaji wa
sheria za uchaguzi, na badala yake watoe taarifa kwenye vyombo vya sheria kwa
hatua stahiki.
Halikadhalika
Makamu wa Rais amesema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu ni muhimu kuendelea
kuwajengea uwezo maafisa na askari kwa kuwapatia mafunzo ya utayari, uadilifu,
na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao. Amempongeza Mkuu wa Jeshi la
Polisi kwa kuendelea kuhakikisha askari wa Jeshi la Polisi wanapata mafunzo ya
kitaalam ya kuwajengea uwezo na utayari.
Kwa upande
wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Daniel Sillo ameishukuru Serikali
ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha
Wizara kibajeti,vifaa na vitendea kazi vya kisasa ambavyo vimesaidia kuimarisha
na kuboresha utendaji wa Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama vilivyopo chini
ya Wizara hiyo.
Ameishukuru
Serikali kwa kutoa vibali vya ajira na upandishaji vyeo hali inayosaidia katika
udhibiti wa uhalifu nchini na kuongeza ari ya utendaji kazi kwa maafisa na askari
ndani ya Wizara. Amesema Wizara na vyombo vyote vya usalama vilivyo chini yake
itaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano, nidhamu, weledi na uadilifu ili
kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama yenye amani na utulivu na mazingira
mazuri kwa ajili maendeleo na uchumi endelevu wa Taifa.
Awali akitoa
taarifa ya Mkutano huo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura
amesema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani
na utulivu na kuwasihi Watanzania wawe na uhakika na utulivu wakiamini kipindi hicho
chote kitapita katika hali ya usalama na utulivu wa hali ya juu pamoja na
Serikali itakayochaguliwa itaingia madarakani bila kikwazo.
Amesema kauli
mbiu inayoongoza mkutano huo inaweka msisitizo katika kusimamia amani na
utulivu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi ili kuhakikisha wananchi
wanashiriki kwa utulivu, uhuru na amani bila kuwa na vikwazo vya aina yeyote.
Pia amesema inasisitiza na kuweka jukumu kwa kila mwananchi kuhakikisha
analinda amani usalama na utulivu kipindi cha kabla, wakati na baada ya
uchaguzi.
Mkutano huo
wa siku tano kuanzia tarehe 11-15 Agosti 2025 unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Amani,
Utulivu na Usalama kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu 2025 ni jukumu letu
sote”