Seneta Miguel Uribe Turbay alipigwa risasi kichwani wakati wa mkutano wa hadhara huko Bogota, Colombia.
Taarifa za kifo cha Uribe (39) zimetolewa na mke wake, Maria Claudia, Jumatatu, 11 Agosti 2025, ambaye amesema kifo hicho kimetokana na mumewe kuvuja damu kwenye mfumo wa neva baada ya kupigwa risasi.
“Alikuwa anatibiwa hapa kwenye Hospitali ya Wakfu wa Santa Fe de Bogota, ambapo ametibiwa kwa mwezi mmoja hadi Jumamosi hali yake ilipobadilika na kuwa mbaya kutokana na tukio la kuvuja damu katika mfumo mkuu wa neva.”
“Namuomba Mungu anipe uwezo wa kuvumilia msiba huu na kuishi bila uwepo wa mume wangu,”amesema Maria alipokuwa akitangaza kifo hicho cha mumewe.
“Naomba Mungu anionyeshe njia ya kujifunza kuishi bila wewe, ameandika Maria Claudia Tarazona, mke wa Uribe kwenye mitandao ya kijamii.
Kifo hicho pia kimemuibua Ivan Duque Marquez, rais wa zamani wa Colombia ambaye amesema kuwa, ugaidi umepokonya kiongozi mwadilifu na muwazi na mpenda maendeleo wa taifa hilo.
“Colombia inaomboleza, lakini haitajisalimisha kwa wahalifu waliochukua maisha ya kijana wa kupendeza, ambaye aliongoza chama cha Democratic Center, kilichokuwa tumaini la wengi, amesema Ivan.
Rais mwingine wa zamani wa nchi hiyo, Alvaro Uribe, amekemea tukio hilo akisema ni uonevu usiovumilika ambao unaharibu taswira ya taifa hilo katika siasa za kimataifa.
“Uovu unaharibu kila kitu, wameua matumaini ya wengi, mapambano dhidi ya unyonyaji na yamepoteza mwanga unaoangazia njia sahihi kwa Colombia.”amesema.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi nchini humo tayari limewakamata watu sita kuhusiana na tukio hilo akiwemo mvulana wa miaka 15 ambaye alishtakiwa kwa jaribio la kuua.
Baadaye mwendesha mashtaka katika kesi hiyo kudai kwamba mtoto huyo alikuwa amezama kwenye mtandao wa wapiganaji ambao pia wamekana mashtaka yalitolewa dhidi yao.
Ikumbukwe kuwe mama mzazi wa Mwanasiasa huyu, Diana Turbay, aliyekuwa mwandishi wa habari pia alitekwa nyara na walanguzi wa dawa za kulevya kutoka kwa genge la Medellin chini ya Pablo Escobar.
Na aliuwawa wakati wa operesheni ya uokoaji mwaka wa 1991 na kupelekea Uribe kulelewa na babake, ambaye alikuwa diwani wa jiji la Bogota.
Mwanasiasa huyu ambaye ni mhitimu wa Harvard, alianza taaluma yake katika siasa za eneo la Bogota, kabla ya kuingia katika Seneti mnamo 2022. Ambapo mwaka jana, katika eneo ambalo mama yake aliuawa, alitangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi wa 2026.
Akiwa na matumaini ya kuipata nafasi hiyo ambayo iliwahi kushikiliwa na babu yake , Julio Cesar Turbay Ayala, aliyewahi kuwa rais kuanzia 1978 hadi 1982, na bibi yake, Nydia Quintero Turbay de Balcazar, aliyekuwa mwanzilishi wa Solidarity with Colombia, kikundi cha wanaharakati kilichotetea na kukuza haki za wafanyakazi nchini humo.