Mkenya Pamba Jiji awashtukia wachezaji

KOCHA Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza amewashtukia wachezaji wa timu hiyo akisema namba yao imekuwa ndogo katika wiki ya kwanza ya maandalizi ya msimu ujao wa mashindano, huku akiweka wazi hiyo inatokana na wengi wao kukimbia mazoezi magumu.

Pamba Jiji imeingia wiki ya pili ya maandalizi tangu imeanza kujifua, huku Baraza akiliambia Mwanaspoti, hajaridhishwa na namba ndogo, lakini waliopo wameonyesha uhai na anatarajia kuwa wataonyesha ushindani mkubwa.

“Maandalizi wiki ya kwanza sio mabaya ila namba ya wachezaji hairidhishi licha ya kuwa na taarifa lakini naamini wachezaji wengi wana tabia ya kutokuhudhuria wiki ya kwanza kutokana na ugumu,” alisema Baraza raia kutoka Kenya aliyeongeza;

“Wiki ya kwanza ni kweli huwa inakuwa na mazoezi magumu lakini yana faida kubwa kwa mchezaji kwani yanawajengea pumzi vizuri na mwili kufunguka baada ya likizo ya muda.”

Baraza alisema amefurahishwa na nyota walioanza pamoja mazoezi kutokana na kuonyeasha jitihada nzuri na anaamini watafanya mambo makubwa msimu ujao huku akiweka wazi kuwa hadi kufikia Jumatano kila mchezaji atatakiwa kuripoti kambini.

“Wiki hii ni ya mwisho kwa wachezaji wote ambao wanatambua wana mkataba na timu hii kuhakikisha wanafika kambini mapema na kuendelea na program ya mazoezi ili kujenga kikosi chenye uwiano mzuri.”

Baraza amejiunga na Pamba Jiji hivi karibuni,  akichukua nafasi ya Fred Felix ‘Minziro’ ambaye ameipambania timu hiyo ibaki ligi kuu na anaongeza idadi ya timu alizofundisha Tanzania baada ya awali kupita Biashara United na Kagera Sugar.