Dar es Salaam. Pigo kwa tasnia ya habari duniani, baada ya mwandishi wa habari wa Al Jazeera, Anas Al-Sharif mwenye umri wa miaka 28 kuuawa kufuatia shambulizi la Israel huko Gaza.
Taarifa ya Al Jazeera iliyochapishwa usiku wa kuamkia leo Jumatatu Agosti 11, 2025 inasema Al-Sharif ameuawa pamoja na wenzake wanne katika shambulio lililolengwa na Israel dhidi ya mahema ya waandishi wa habari katika mji wa Gaza.
“Watu saba waliuawa katika shambulizi dhidi ya hema lililoko nje ya lango kuu la Hospitali ya Al-Shifa ya Gaza Jumapili jioni. Ni pamoja na mwandishi wa Al Jazeera Mohammed Qreiqeh na watu wa kamera Ibrahim Zaher, Mohammed Noufal na Moamen Aliwa,” imeeleza taarifa hiyo.
Muda mfupi kabla ya kuuawa, Al-Sharif, mwandishi huyo mashuhuri wa Kiarabu wa Al Jazeera aliandika kwenye mtandao wa X kwamba Israel ilikuwa imeanzisha mashambulizi makali ya mabomu.
Katika ujumbe wa mwisho, ulioandikwa Aprili 6, Al-Sharif alisema alipitia maumivu makali pamoja na huzuni katika maisha yake ya huko Gaza.
“Pamoja na hayo, sikusita kamwe kueleza ukweli jinsi ulivyo, bila upotoshaji, nikitumaini kwamba Mungu angeshuhudia wale waliokaa kimya, wale waliokubali mauaji yetu, na wale ambao waliziba pumzi,” aliandika na kuongeza.
“Hata miili iliyoharibiwa ya watoto wetu na wanawake haikugusa mioyo yao au kukomesha mauaji ambayo watu wetu wamekuwa wakifanyiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu.”
Mwandishi huyo pia alieleza masikitiko yake kwa kumwacha mkewe, Bayan, na kutomwona mwanaye, Salah na binti yake, Sham wakiwa wanakua.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mtandao wa vyombo vya habari wa Al Jazeera umelaani mauaji hayo kama; “Shambulio jingine la wazi na la kukusudia dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.”
Shambulio hilo linakuja huku kukiwa na matokeo mabaya ya mashambulizi yanayoendelea ya Israel huko Gaza, ambayo yameshuhudia mauaji ya raia, njaa ya kulazimishwa na kuangamiza jamii nzima.
“Amri ya kumuua Anas Al Sharif, mmoja wa waandishi wa habari shupavu wa Gaza, na wenzake, ni jaribio la kukata tamaa la kunyamazisha sauti zinazofichua kutekwa na kukaliwa kwa Gaza.”
Al Jazeera ilitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na mashirika yote husika kuchukua hatua madhubuti kukomesha mauaji haya ya kimbari yanayoendelea na kukomesha ulengaji wa makusudi wa waandishi wa habari.
“Al Jazeera inasisitiza kuwa kinga kwa wahalifu na ukosefu wa uwajibikaji hutia moyo vitendo vya Israel na kuhimiza ukandamizaji zaidi dhidi ya mashahidi wa ukweli,” mtandao huo ulisema.
Mwandishi wa Al Jazeera Hani Mahmoud, ambaye alikuwa umbali wa mtaa mmoja tu wakati wa shambulizi linatokea, amesema kuripoti kifo cha Al-Sharif lilikuwa jambo gumu zaidi ambalo amelazimika kufanya katika miezi 22 iliyopita ya vita.
Mahmoud, ambaye anafanya kazi katika idhaa ya Kiingereza ya mtandao huo, amesema waandishi hao waliuawa kwa sababu ya kuripoti kwao bila kuchoka juu ya njaa na utapiamlo, unaowatesa Wapalestina huko Gaza, “kwa sababu wanasema ukweli wa uhalifu huo.
Muhammed Shehada, mchambuzi katika Shirika la Kufuatilia Haki za Kibinadamu la Euro-Med, amesema hakuna ushahidi kwamba Al-Sharif alishiriki katika uhasama wowote.
“Maisha yake yote ya kila siku yalikuwa yamesimama mbele ya kamera kutoka asubuhi hadi jioni,” ameiambia Al Jazeera.
Tangu Israel ilipoanzisha vita vyake dhidi ya eneo hilo mnamo Oktoba 2023, mara kwa mara imekuwa ikiwashutumu waandishi wa habari wa Kipalestina huko Gaza kuwa wanachama wa Hamas, kama sehemu ya kile ambacho mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema ni jitihada za kudharau ripoti zao za dhuluma za Israel.
Jeshi la Israel limewaua zaidi ya waandishi 200 na wafanyakazi wa vyombo vya habari tangu mashambulizi yake yalipoanza, wakiwemo wanahabari kadhaa wa Al Jazeera na jamaa zao.