RAIS wa Kenya William Ruto ametoa ahadi ya Sh2.5 milion za Kenya (sawa na Sh47 milioni za Tanzania) endapo Harambee Stars itashinda dhidi ya Zambia Jumapili, kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi ‘A’ wa michuano Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) 2024, Uwanja wa Moi International Sports Centre, Kasarani.
Pia ametoa ahadi ya nyumba ya vyumba viwili kwa kila mchezaji endapo watatinga nusu fainali na endapo watafika fainali watapata nyumba ya vyumba vitatu kila mmoja.
Ruto ameyasema hayo alipofanya kikao na wachezaji timu ya taifa ya Kenya, leo Jumatatu katika Hoteli ya Pullman, Upper Hill, Nairobi.
Pia alitumia nafasi hiyo kuwapongeza nyota huyo baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Morocco kwenye Kundi ‘A’ Jumapili katika uwanja huo wa Kasarani na kuwakabidhi Sh804 milioni kwa kikosi hicho.
Ruto pia alitimiza ahadi yake ya kuwazawadia Sh1 milioni ambayo ni sawa na milion 19 za kitanzania kila mmoja wa wachezaji 42 wa Harambee Stars kwa kila ushindi katika CHAN 2024, na Sh500,000 (milion 9 kwa Tanzania) kwa kila sare watakayopata kwenye mashindano ambayo Kenya inaandaa kwa ushirikiano na Tanzania na Uganda.
“Nipo hapa pia kutimiza ahadi yangu. Tulikubaliana mkifanya sehemu vizuri nitawazawadia kama nilivyoahidi,” alisema Rais Ruto kabla ya kutangaza motisha mpya kwa michezo ijayo.
“Mkiishinda Zambia, kila mmoja wenu atapata Sh2.5 milioni,” amesema Ruto huku akishangiliwa na kupigiwa makofi na wachezaji.
Rais pia alijibu ombi la kikosi hicho kuhusu kupewa nafasi ya kupata nyumba kupitia mradi wa Nyumba Nafuu.
“Mkiibuka na ushindi robo fainali, kila mmoja wenu atapata Sh1 milioni (milion 9 kwa Tanzania) na nyumba ya vyumba viwili,” amesema Ruto. “Mkishinda nusu fainali, kila mmoja atapata Sh1 milioni (milion 9 kwa Tanzania) na nyumba ya vyumba vitatu,” ameongeza Rais.
Ushindi dhidi ya Morocco ulikuwa wa kwanza kwa Harambee Stars dhidi ya Atlas Lions, baada ya kupoteza mara tatu na kutoka sare mara mbili katika mechi tano zilizopita. Pia ushindi huo uliivunja rekodi ya Morocco ya kutopoteza michezo 14 mfululizo kwenye michuano ya CHAN.
Mshambuliaji wa Tusker FC, Ryan Ogam, alifunga bao pekee la Kenya dakika ya 42, huku kipa Byrne Omondi akiibuka mchezaji bora wa mechi baada ya kulinda vyema uongozi wa Harambee Stars kufuatia kutolewa kwa kadi nyekundu kwa beki Chrispine Erambo wa Tusker dakika ya 45.