Kongwa. Mwili wa Spika wa Bunge mstaafu Job Ndugai umezikwa leo Agosti 11, 2025 shambani kwake, katika Kijiji cha Mandumbwa Kata ya Sejeli wilayani Kongwa huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongoza waombolezaji kwenye mazishi hayo na kutoa ujumbe wa kumuenzi.
Wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Zena Saidi, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, John Mongela, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, viongozi wengine kitaifa, ndugu, jamaa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Akizungumza kwenye mazishi hayo, Majaliwa amesema Serikali itatekeleza miradi yote iliyoanzishwa na Ndugai ikiwamo ya kuitangaza Wilaya ya Kongwa kuwa kitovu cha wapigania uhuru kwa nchi za kusini mwa Afrika.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwa taasisi zinazohusika kuhakikisha miradi yote ya maendeleo iliyoanzishwa na Ndugai inakamilika.
”Napenda kuchukua nafasi hii kuwaambia kuwa, tutasimamia miradi yote iliyoanzishwa na Spika mstaafu wilayani Kongwa jambo ambalo alikuwa amelianzisha na kulisimamia,” amesema.
Majaliwa amewataka Watanzania kuenzi mema yote yaliyofanywa na Ndugai, akisema mchango wake katika uongozi wa Bunge na Taifa kwa jumla utabaki kuwa kumbukumbu muhimu kwa vizazi vijavyo.

Amesema akiwa mwakilishi wa wananchi wa Kongwa, Ndugai ametoa mchango mkubwa katika kipindi cha miaka 20 ya utumishi wake na kwamba, wote ni mashuhuda wa maendeleo yaliyopatikana katika sekta mbalimbali za maendeleo pamoja na huduma za kijamii.
“Serikali itaendelea kumuenzi kwa yale yote aliyoyafanya kwa wana Kongwa,”amesema Majaliwa.
Amesema Ndugai alikuwa mlinzi wa taratibu za Bunge na mshirika wa karibu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Bunge na Serikali kwa masilahi mapana ya Taifa, akisisitiza mawasiliano ya uwazi, mshikamano na mwelekeo wa pamoja wa utekelezaji wa ajenda za kitaifa.
Pia, Majaliwa amemtaja Ndugai kama kiongozi aliyekuwa na weledi, uadilifu, unyenyekevu na mchapakazi aliyebeba heshima ya Mkoa wa Dodoma na Jimbo la Kongwa kupitia uongozi na siasa za uwajibikaji.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema msiba wa Ndugai ni mzito huku akiwataka wana Kongwa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kumpoteza kiongozi huyo.
Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema wanaamini katika kumuenzi Ndugai na watamkumbuka kwa kuendeleza mema yote aliyoyatenda.
Kwenye ibada ya mazishi katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Michael Kongwa, Askofu mkuu wa kanisa hilo Maimbo Mndolwa amesema Ndugai alitumia vizuri talanta alizopewa na Mungu hapa duniani, kuanzia ya uongozi, familia, huduma ya kanisa na jamii.
Amesema Ndugai alitumia talanta yake kwa sababu mambo aliyoyafanya na kuyaanzisha yanaonekana ndani na nje ya nchi.
”Sijui alipewa talanta ngapi na Mungu, tano, tatu au moja, lakini amezitumia vizuri hakuzificha kwa sababu zinaonekana kupitia taaluma yake, watoto na wajukuu, huduma za kanisa na jamii na uongozi wake alipokuwa mbunge, Spika wa Bunge na hata kimataifa,” amesema Askofu Mndolwa.

Askofu Mndolwa amesema pia alikuwa na ulimi wenye kauli nzuri na hata alipokuwa anazungumza alionekana kumaanisha maneno yake, hivyo alitumika kutatua changamoto mbalimbali ndani na nje ya kanisa.
Wakazi wa Wilaya ya Kongwa wamejitokeza kwa wingi kwenye mazishi ya Ndugai aliyezikwa shambani kwake Kijiji cha Mandumbwa Kata ya Sejeli Wilayani humo.
Pia, baadhi ya watu walijitokeza barabarani kumuaga Ndugai wakati mwili wake ukitolewa kanisani kuelekea shambani kwake kuzikwa.
Watu hao wakubwa kwa wadogo wenye sura za huzuni, walijitokeza na kupungia mkono msafara wa magari uliokuwa unaelekea makaburini.
Wakizungumza na Mwananchi, wakazi hao wamesema wamempoteza kiongozi waliyempenda na kuwasaidia kwenye shida na raha.
Lameck Nyau, amesema Ndugai alikuwa msaada kwa wakazi wa Kongwa kwa sababu aliwasaidia kuwasomesha watoto wao pale walipokwama kuendelea na shule kwa kukosa ada na mahitaji mengine ya shule.
”Alikuwa kiongozi mzuri, msiba wake umetushtua wote kwa kweli tuna huzuni sana,” amesema Nyau.
Naye, Sechelela Yolam amesema msiba wa Ndugai ni pigo kwa wana Kongwa kwa sababu walikuwa bado wanamuhitaji kuwaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
”Nimekuja hapa kushuhudia mazishi yake ili niamini kweli kiongozi wangu amefariki, kwa kweli nimeumia sana,” amesema Yolam.
Mkazi mwingine wa Kongwa, Yohana Mlule amesema msiba wa kiongozi huyo ni pigo kwao kwa sababu alikuwa kiongozi msikivu na alishirikiana naye kutatua changamoto mbalimbali zilizowakabili.