Moshi. Ikiwa zimepita siku 407 tangu kutoweka kwa muuguzi wa idara ya masikio, pua na koo (ENT), Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC, Lenga Masunga Ng’hajabu (38) familia imesema bado hawajakata tamaa kumtafuta.
Muuguzi huyo anadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Julai 2, mwaka 2024, mtaa wa Rau Pangaleni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro alikokuwa akiishi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na hospitali ya KCMC, Masunga alikuwa mapumziko ya siku mbili (off), Julai 2 na 3 na kwamba alitakiwa kuwepo kazini Julai 4, mwaka huo baada ya likizo yake kumalizika lakini hakuonekana hali ambayo iliibua mashaka na kusababisha uongozi wa hospitali hiyo kumtafuta kupitia simu zake za mkononi ambazo hazikupatikana mpaka leo.
Taarifa ya kutoweka kwake ilitolewa katika Kituo cha Polisi Longuo, kilichopo Wilaya ya Moshi na kutolewa RB namba LNG/RB/33/2024 kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo, Agosti 11, 2025 kaka wa muuguzi huyo, Paschal Jeremiah amesema licha ya kuhangaika kwa muda mrefu familia bado wana imani ipo siku atapatikana iwe amekufa au akiwa hai.
“Bado hatujampata, tumehangaika kumtafuta mpaka tumechoka, kama yupo hai au amekufa Mungu ndiye anayejua hatuna njia nyingine ya kumtafuta maana imekuwa kazi ngumu sana,”amesema.
Amesema hali hiyo imekuwa ikiwatesa wanafamilia hasa mama yake ambaye ni mzee na ni mgonjwa.
“Mama amekuwa hapati usingizi akiwaza mwanaye alivyotoweka katika mazingira ambayo hayaelewi mpaka sasa, tumehangaika vya kutosha lakini hatujafanikiwa chochote mpaka sasa,”amesema kaka huyo.
Akizungumza na Mwananchi leo, Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Gabriel Chisseo amesema bado wanaendelea kumtafuta na taarifa zote zipo katika mamlaka husika kuhusu.
“Taarifa tulizikabidhi kwa Jeshi la Polisi na kwa ndugu zake ambao walikuja hapa KCMC, hata sisi pia bado tunahangaika sana kumtafuta,”amesema Chisseo