SportPesa kuipa Yanga 21.7 bilioni

Kama unadhani ndoa ya Yanga na kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa itaishia njiani unakosea. Pande hizo mbili zimesaini mkataba mpya wenye thamani ya Sh21.7 bilioni.

Ilikuwa Julai 27, 2022 ambapo pande hizo ziliingia mkataba wa miaka mitatu  uliokuwa na thamani ya Sh12.3 bilioni uliomalizika mwisho wa msimu uliopita.

Mkataba mpya ambao umesainiwa leo umekuwa na ongezeko la Sh9.4 bilioni utakaifanya  SportPesa kuendelea kukaa mbele ya jezi za mabingwa hao.

Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa SportPesa, Abbas Tarimba amesema safari ya udhamini wao kwa Yanga ni kutokana na kuamini kwamba ni timu sahihi yenye mashabiki wengi na kwamba itaweza kubadili mpira wa Tanzania.

“Tumewahi kudhamini klabu nyingi kubwa zikiwemo Arsenal, Hull City, Everton na ligi ya Kenya, lakini hapa Tanzania tuliiona Yanga ndio klabu sahihi ambayo tunaweza kufanya nayo kazi ili waubadilishe mpira wa Tanzania,” amesema Tarimba.

“Tulipoingia Yanga tuliwapa nguvu ya kiuchumi, ndio maana mnaona sasa Yanga inaweza kumuuza mchezaji yeyote na inaweza kununua mchezaji yeyote. Kwenye mkataba huu tumeweka kiwango kikubwa cha fedha ambacho kwa kuwa Yanga wanataka kushinda ubingwa wa Afrika basi kiasi hiki kitawafanya kupambana ili wakiupata watajipatia.”

Rais wa Yanga, Hersi Said ameipongeza SportPesa kwa kuipa nguvu ya kiuchumi  timu hiyo akisema imeisaidia kubadilisha mambo mengi ndani ya klabu hiyo.

“Tunawapongeza sana SportPesa kwa kuipa klabu hii nguvu kubwa ya kiuchumi miaka ya nyuma licha ya ukongwe wa Yanga, kuna nyakati ilikuwa unashindwa kuendesha mambo, kusajili wachezaji, kumudu gharama za uendeshaji wapo wachezaji waligoma kuja kujiunga na timu kutokana ukosefu wa fedha,” amesema Hersi.

“Hali hiyo haipo sasa. Yanga ya sasa inaweza kupambana na klabu yoyote kubwa na kuwania mchezaji na ikampata. Wapo wachezaji waliacha ofa za klabu zingine wakaja Yanga. Hawakuja hapa kwa mapenzi yao kwa klabu ni kutokana na  ushawishi wa fedha.”

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Khamis Mwinjuma ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo amezipongeza Yanga na SportPesa kwa kudumu miaka minane katika ushirikiano huo.

Hafla hiyo imefanyika Hoteli ya Serena imehudhuriwa na viongozi wengine wa Yanga, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Makamu wa Rais, Athuman Nyamlani, kikosi cha Yanga na benchi la ufundi.