Dar es Salaam. Hali ya taharuki imetokea katika machinjio ya Ukonga Mazizini baada ya askari magereza zaidi ya 20 wanaodhaniwa ni wa Gereza la Ukonga, kudaiwa kuvamia eneo hilo na kupiga wafanyakazi wa machinjio
Hata hivyo mkuu wa Gereza la Ukonga, Juma Mwaibako amesema hana taarifa za askari wake kufanya vurugu hizo akisisitiza kwamba huenda tukio hilo lipo lakini halijafanyika katika eneo lake.
“Ukonga ni kubwa, binafsi sina taarifa hizo, zifuatilie vizuri inaweza kuwa limetokea lakini sio kwangu,” amesema mkuu huyo kwa kifupi.
Akizungumzia tukio lilivyokuwa, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mifugo machinjioni hapo, Shedrack Mahende amesema taharuki hiyo ilianza jana Jumapili kuanzia saa 4 asubuhi.
“Askari magereza wa Ukonga zaidi ya 20 walifika hapa machinjioni na kuanza kupiga watu, wengine wakifanya uporaji na uharibifu wa ofisi za machinjio kwa madai kwamba wanatafuta watu ambao wamefanya mauaji ya askari magereza mwenzao,” amesema Mahende.
Amesema tukio la askari huyo kuuwawa lilitokea usiku wa kuamkia jana Jumapili Agosti 10, 2025 nje ya machinjio hiyo iliyopo Mtaa wa Ukonga Mazizini.
“Hakuuawa hapa machinjioni, ni nje ya machinjio na haijajulikana chanzo cha kifo chake, lakini askari magereza wenzake walikuja hapa machinjioni na kufanya uharibifu wa mali na kupiga watu,” amesema.
Amesema vijana sita ambao ni wafanyakazi kwenye machinjio hiyo walikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Sitaki Shari.

“Vurugu zilipoongezeka, uongozi wa machinjio tuliomba msaada kwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), ambapo alituma askari na kufanya doria usiku kucha machinjioni hapa.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Sitaki Shari alipotafutwa, simu yake ilipokelewa mara kadhaa na mwandishi alipojitambulisha alikata simu na kisha simu hiyo haikupokelewa tena.
Mjumbe na mshauri mkuu wa chama cha wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake katika machinjio ya Ukonga Mazizini, Nestory Lukaya amesema taharuki hiyo imesababisha biashara kutofanyika kuanzia jana hadi leo Jumatatu.
“Kwa asilimia kubwa kazi hazikufanyika hapa machinjioni, tupo katika hamaki kwani mifugo huanza kuingia machinjioni kuanzia saa 4:00 asubuhi, lakini kutokana na taharuki hiyo hakuna kilichofanyika,” amesema.
Amesema mbali na mifugo kuingia, kazi ndani ya machinjio huanza saa 6:00 usiku hadi saa 2:00 asubuhi lakini kutokana na taharuki hiyo nayo haikuendelea.
“Askari Magereza wale walikuwa wanakuja wanashambulia na kuondoka, baada ya muda wanarudi tena, tuliomba msaada wa polisi na ndiyo walitusaidia kupiga simu kituo chao cha kazi wazuiwe, hata hivyo bado hatukuweza kuingia kazini kwa hofu,” amedai.
Hata hivyo OCD alipotafutwa na kuulizwa juu ya tukio hilo, alihoji ni wapi mwandishi anapata taarifa za polisi na kutaka atafutwe Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.
“Huyo ndiye msemaji, mtafute yeye umuulize, mimi sina cha kukujibu,” amesema OCD huyo kwa kifupi na kukata simu.
Mwananchi ilimtafuta Kamanda Muliro ambaye simu yake binafsi na ya ofisi zote hazikupokelewa.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Ukonga Mazizini, Musa Komba amekiri kutokea kwa taharuki hiyo mtaani kwake akibainisha kwamba zilitokea jana asubuhi na uongozi wa mtaa ulipiga simu kikosini wanapotoka askari hao.

Amesema hadi kufikia leo Agosti 11, saa 5:00 asubuhi hali ilikuwa imetulia, japo bado shughuli za machinjio hazikuwa zimeendelea kutokana na taharuki iliyokuwepo jana.
“Taarifa ambazo nilipewa ni kwamba mkuu wa kikosi amewazuia na sasa hali ya taharuki imetulia,” amedai kiongozi huyo wa mtaa.
Amedai chanzo cha askari Magereza hao kwenda kufanya fujo na kupiga raia kulitokana na hamaki ya tukio la mwenzao kufariki kwa kuuwawa na watu wasiojulikana.
“Taarifa ambazo tumezisikia ni kwamba alikuwa katika unywaji, inasemekana walikuwa wanagombania mwanamke, katika mazingira waliyokuwepo ndipo akajeruhiwa na kusababisha kifo chake.
“Huku kwetu kuna shughuli za uchinjaji ng’ombe, wenzetu wakimaliza kazi silaha zile huwa nazo, baada ya kutoelewana mtu waliyekuwa wakizozana aliitumia kumjeruhi na kusababisha kifo cha askari magereza huyo,” amedai.
Amedai mama wa binti ambaye walikuwa wakimgombania tayari amekamatwa na kueleza taarifa zaidi wanazo jeshi la polisi.