Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeongeza muda kujisajili kulipa kodi kwa watu binafsi na taasisi zote zinazojihusisha na biashara mtandao, sasa ukomo wake hadi Desemba 31, 2025 kutoka Agosti 31.
Nyongeza ya muda huo, haiwahusu, wafanyabiashara wakubwa wanaofanya biashara ya kupangisha nyumba kupitia mitandao, wamiliki na waendeshaji wa majukwaa ya kidijitali ambapo ukomo wao ni Agosti 31, 2025.
Julai 24, Kamishna Mkuu wa TRA alitoa tangazo kuwa wafanyabiashara wote wa mtandaoni kujiandikisha na kujisajili ndani ya siku 30, kuanzia Agosti Mosi hadi Agosti 31,2025.
Katika kuweka msisitizo wa muda huo na uliongezwa, TRA imewasihi wafanyabiashara hao na makundi yote kuzingatia muda huo, akiweka wazi kuwa watakaokiuka matakwa hayo ya sheria watatoza faini na adhabu.
Taarifa iliyotolewa kwa umma na mamlaka hiyo kutoka Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano, imeeleza ongezeko hilo la muda kwa kundi hilo kujisajili kutokana na maombi ya baadhi ya wafanyabiashara wa kati na wadogo.
“Wameomba kuongezewa muda wa kutosha wa kuwasikiliza wafanyabiashara wote wa mtandaoni, kutoa elimu ya kodi pamoja na kuandaa mifumo itakayorahisisha utekelezaji wake na kuondoa usumbufu kwa walipakodi,” imesema taarifa hiyo.
Kulingana na taarifa hiyo, wafanyabiashara wakubwa wanaofanya biashara ya kupangisha nyumba kupitia mitandao kama vile Airbnb, Booking.com, Agoda, Expedia hawataongezewa muda.
“Wengine wasioongozewa muda ni pamoja na wamiliki na waendeshaji wa majukwaa ya kidijitali (Digital Platforms), hawa wanatakiwa kujisajili ndani ya muda uleule uliotolewa awali wa hadi kufikia Agosti31,2025,” imeeleza taarifa hiyo.
Imeeleza watu binafsi na taasisi zote zinazojihusisha na biashara kupitia mtandao kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Kodi ya Mapato (Sura 332), mtu yeyote anayepata kipato kutokana na biashara, uwekezaji au ajira anawajibika kisheria kulipa kodi.
“Wajibu huu unahusu pia shughuli zote za biashara za kidijitali, zikiwemo kuuza bidhaa (za ndani, nje au duniani kote) na kutoa huduma kupitia mtandao,”imefafanua.
Ili kutimiza matakwa haya ya kisheria, TRA imeeleza kuwa waendeshaji wote wa biashara za mtandaoni wanatakiwa kujisajili na kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), kama inavyoelekezwa na kifungu cha 22 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi (Sura 438).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TRA imesema wafanyabiashara wote wana wajibu wa kujisajili, kuwasilisha ritani na kulipa kodi kutokana na mapato yao.
“Kwa wafanyabiashara wanaopata kipato kupitia miamala ya kidijitali ambacho kina mauzo (turnover) ya zaidi ya sh4 milioni na hawajasajiliwa na TRA, na inayolenga walaji wa Tanzania, wanapaswa kujisajili na kulipa kodi stahiki hata kama hawana ofisi, duka au ghala lililosajiliwa hapa nchini,”imesisitiza
Imetaja biashara hizo za mtandaoni zinajumuisha shughuli mbalimbali ikiwemo watu binafsi wanaouza bidhaa kupitia mitandao kama Instagram, Facebook, WhatsApp Business, Tik Tok, X (zamani Twitter), Jamiiforums, Jiji na mingineyo.
“Wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) wanaofanya biashara za mtandaoni kupitia masoko ya kidijitali au tovuti zao binafsi, wamiliki wa mali au watu binafsi wanaotoa huduma za upangishaji wa nyumba kwa muda mfupi kupitia majukwaa kama vile Airbnb.
“Na huduma nyingine za upangishaji kwa njia ya mtandao na kujipatia kipato, hata kama hawana ofisi au makazi ya kibiashara yaliyo rasmi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.