Mbeya. Katika jitihada za kuboresha uzalishaji wa maziwa na kuinua sekta ya mifugo, wafugaji katika Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, wameanza kutumia teknolojia za kisasa za uhimilishaji wa majike ya ng’ombe kwa kutumia mbegu bora.
Ofisa Uhimilishaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Haji Ludanga amesema kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yameanza kuleta mafanikio makubwa kwa wafugaji, ikiwemo ongezeko la ng’ombe wenye uwezo mkubwa wa kuzalisha maziwa, licha ya changamoto ndogo zinazojitokeza katika mwenendo wa takwimu za uzalishaji.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Agosti 11, 2025, Ludanga amesema kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuboresha kizazi cha mifugo na kuhakikisha kuwa wafugaji wanapata tija zaidi kutokana na shughuli zao.
“Pamoja na changamoto za kupanda na kushuka kwa takwimu za uzalishaji, tumeona matokeo chanya kwenye ubora wa ndama wanaozaliwa na kiwango cha maziwa kinachopatikana,” amesema Ludanga.
Ameongeza kuwa elimu kwa wafugaji kuhusu matumizi ya teknolojia hizo inaendelea kutolewa kwa kushirikiana na maofisa ugani, taasisi za utafiti wa mifugo na wadau wengine wa maendeleo vijijini.
“Kimsingi takwimu zinapanda na kushuka ambapo kwa mwaka 2020/2021 majike 4,188 yalihimilishwa kati ya hao 1,591 yalipata mimba, lakini mwaka 2021/ 2022, majike 4,461 yalihimilishwa 1,714 yalipata mimba,” amesema.
Amesema kwa mwaka 2022/23 5,893 yalihimilishwa 2,239 yalishika mimba, na mwaka 2023/24, takwimu zilishuka ambapo 4,637 yalihimilishwa huku 1,908 yalishika mimba, kwa 2024/2025, takwimu zilipanda na kufikia 4,908 huku 1,873 yalishika mimba.
Ludanga ametaja changamoto ya kupanda na kushuka kwa takwimu ni kutokana na baadhi ya wafugaji kutokuwa na taarifa sahihi za mifugo za kupata joto.
Kwa upande wake Ofisa Mifugo Kata ya Lufingo Wilaya ya Rungwe, Zainab Mwamba amesema mwaka 2020/25 uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka wastani wa lita 48,339 hadi 64,800 sawa ya ongezeko la asilimia 10 kwa kila mwaka.
Ametaja sababu ni ongezeko la uzalishaji zao la maziwa kuwa ni pamoja na kuelimisha wafugaji jinsi ya kutumia mifumo ya uhimilishaji kupandisha majike ili kupata kizazi bora kwa ajili ya manufaa yao kiuchumi.
“Uhimilishaji wa kutumia njia ya chupa unasaidia kupandikiza mbegu nzuri ambazo zimetoka kwa dume bora zilizochujwa na kupimwa na wataalamu na kupelekea kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Amesema asilimia 90 ya ng’ombe wilayani humo wamepandikizwa kwa njia ya uhimilishaji na kuleta tija kubwa na mpaka sasa wafugaji 20,000 wamepata elimu.
Mfugaji Kata ya Kandete, Frank Mwakyangwe amesema kimsingi uhimilishaji wa mifugo umeleta tija kubwa kwao katika suala la uzalishaji maziwa bora na uchumi wao kukua.